Waziri wa Fedha wa Marekani asema lazima Bunge lipandishe kikomo cha deni ifikapo Oktoba 18

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 30, 2021
Waziri wa Fedha wa Marekani asema lazima Bunge lipandishe kikomo cha deni ifikapo Oktoba 18

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen Jumanne hii amesema kwamba wabunge wanatakiwa kupandisha au kusimamisha kikomo cha deni hadi kufikia Oktoba 18 mwaka huu ili kuepuka nchi hiyo kushindwa kulipa deni lake.  

“Kwa sasa tunakadiria kwamba wizara ya fedha italazimika kuchukua hatua zake za dharura kama bunge halitachukua hatua za kuongeza au kusimamisha kikomo cha deni ifikapo Oktoba 18” Yellen alisema katika barua aliyowaandikia viongozi wa bunge.

“Katika hatua hiyo, tunatarajia kwamba wizara ya fedha itakuwa imebakiwa na rasilimali zisizotosha ambazo nazo zitaisha kwa haraka. Hakuna uhakika kama tutaendelea kukidhi mahitaji yote ya Serikali baada ya tarehe hiyo” alisema.

Yellen alisisitiza kwamba Bunge halipaswi kusubiri hadi muda wa mwisho kuongeza kikomo cha deni kwani makadirio juu ya hatua za muda mfupi zilizochukuliwa na fedha taslimu zinaweza kudumu kwa muda gani unaweza kubadilika bila kutarajia.

“Tunafahamu kutokana na uzoefu wa tatizo hili huko nyuma kwamba kusubiri hadi muda wa mwisho kunaweza kusababisha madhara makubwa kwenye hali ya kujiamini kwa makampuni na watumiaji bidhaa, kuongeza gharama za kukopa kwa walipa kodi na kuleta athari za muda mrefu kwenye kiwango cha mkopo katika miaka kadhaa ijayo” alisema huku akiongeza kwamba kushindwa kwa bunge kuchukua hatua stahiki kutaleta msukosuko katika soko la fedha kwani kukosekana uhakika kunaweza kusababisha kuyumba na kubomoa hali ya kujiaminika kwa wawekezaji.

Barua hii ya Yellen imeandikwa baada ya wabunge wa chama cha Republican wakiongozwa na Seneta Mitch McConnell kupiga kura ya veto kuzuia hatua za kutoa fedha kwa serikali kuu na kuondoa kikomo cha deni Jumatatu jioni.

Kama sehemu ya makubaliano ya bajeti ya pande zote za Democrats na Republicans yaliyofikiwa Mwezi Agosti, 2019, Bunge liliondoa kikomo cha deni hadi Julai 31 mwaka huu. Baada ya kikomo cha deni kurejeshwa tena Agosti 1 mwaka huu, Wizara ya Fedha ilianza kuchukua “hatua zisizo za kawaida” kuendelea kugharamia matumizi ya Serikali.

Kikomo cha deni, ni jumla ya kiasi cha fedha ambacho Serikali Kuu ya Marekani inaidhinishwa kukopa ili kukidhi majukumu yake ya kisheria ikiwemo usalama wa jamii na huduma za afya, riba kwenye deni la taifa na malipo mengine.  

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha