Tunisia kuanza kutoa dozi ya tatu ya chanjo ya UVIKO-19 kwa wazee

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 30, 2021

Kamati ya kisayansi ya kupambana na virusi vya korona nchini Tunisia Jumanne ya wiki hii iliidhinisha kutoa dozi ya tatu ya chanjo ya UVIKO-19 kwa raia wenye umri wa miaka 75 na zaidi.

Zoezi hili la utoaji dozi ya tatu ya chanjo litaanza katika kipindi kijacho, Jalila Ben Khelil, msemaji wa kamati hiyo alinukuliwa na Shirika la Habari la Tunisia na Afrika (TAP).

“Baada ya kundi hili, kampeni hii italenga kundi la raia wenye umri wa zaidi ya miaka 50” Alisema Khelil.

Dozi ya tatu dhidi ya UVIKO-19 itatolewa pia kwa wale wenye magonjwa sugu ambayo yanaathiri kinga ya mwili, na pia wataalamu wa afya ambao walidungwa chanjo ya kwanza mwezi Machi mwaka 2021, Khelil alisema.

Idadi ya vifo vinavyotokana na janga la UVIKO-19 nchini Tunisia iliongezeka na kufikia watu 24,794 baada ya wagonjwa wengine 6 kufariki, wizara ilisema.

Tangu kuanza kwa zoezi la utoaji chanjo tarehe 13, Machi, 2021 jumla ya watu 3,968,319 nchini Tunisia wameshakamilisha kudungwa chanjo dhidi ya UVIKO-19. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha