Utafiti waonyesha hatua za udhibiti wa mlipuko wa UVIKO-19 zaharibu biashara ndogo Afrika Kusini

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 30, 2021

Hatua mbalimbali za udhibiti wa maambukizi ya UVIKO-19 zimeleta athari kubwa kwenye biashara ndogo-ndogo na sekta isiyo rasmi nchini Afrika Kusini huku ajira zaidi ya milioni 3 zikipotea, ripoti ya utafiti iliyotolewa Jumanne ya wiki hii imeeleza.

Utafiti huo wenye kichwa “Athari za UVIKO-19 juu ya Biashara ndogo-ndogo na zisizo rasmi nchini Afrika Kusini” ulifanywa na Idara ya Biashara ndogo-ndogo kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)

“Mlipuko wa UVIKO-19 na ufungiaji watu ndani ili kuzuia maambukizi ya virusi vya korona ulikuwa wa kiwango kikubwa na umeelezwa kuwa wenye changamoto zaidi kuliko msukosuko wa uchumi uliotokea miaka 10 iliyopita” Ripoti inasema.

Sekta isiyo rasmi ambayo ilichukua asilimia 8 ya ukuaji wa jumla wa uchumi wa Afrika Kusini na yenye kuajiri asilimia 27 ya nguvukazi iliathiriwa zaidi, ripoti inasema.

Utafiti pia umeonesha, biashara ndogo na zisizo rasmi ambazo zilifunguliwa tena wakati hatua za kufungia watu ndani kulegezwa zilishindwa kurejea katika hali yake ya mapato au idadi ya ajira zilizopatikana kabla ya janga la korona.

Wakati janga hili linaathiri sekta nyingi za uchumi, athari zilikuwa kubwa zaidi katika baadhi ya maeneo hasa ya sekta za ujenzi, huduma, chakula na vinywaji baridi.

Wanawake pia waliathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga hili, huku ajira nyingi zikipotea, ripoti ilieleza zaidi.

Ripoti hiyo imebaini kwamba, wakati serikali ilitoa msaada wa kifedha kupunguza makali ya athari za janga hili, msaada huu ulijikita zaidi katika biashara rasmi. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha