Mkutano wa pili wa Usafirishaji Endelevu wa UN wahitimishwa na Azimio la Beijing

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 18, 2021
Mkutano wa pili wa Usafirishaji Endelevu wa UN wahitimishwa na Azimio la Beijing
Mkutano wa Pili wa Usafirishaji Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UN) wafungwa Jijini Beijing, Mji Mkuu wa China, Oktoba 16, 2021. (Xinhua / Li He)

BEIJING - Mkutano wa Pili wa Usafirishaji Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UN) umefungwa jijini Beijing, China Jumamosi ya wiki iliyopita, huku Azimio kuhusu matokeo ya mkutano huo likitolewa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa usafirishaji endelevu, azimio hilo limesisitiza kwamba kuharakisha mabadiliko kuelekea usafiri endelevu itakuwa muhimu katika kujenga jamii yenye mustakabali wa pamoja kwa binadamu.

"Teknolojia mpya na zinazoibuka zinapotumika vizuri, ni muhimu katika kutatua changamoto nyingi kwa usafirishaji endelevu," linaelewa kwenye azimio hilo, likihimiza ushirikiano wa kimataifa, kujenga uwezo na kubadilishana maarifa kati ya nchi mbalimbali.

Mahitaji ya jamii za vijijini zilizo pembezoni na nchi zilizo katika hali maalum yanapaswa kushughulikiwa kwa kupanua mifumo endelevu ya usafirishaji na miundombinu. Jitihada pia zinapaswa kufanywa katika kuongeza usalama wa barabara, na kuboresha uwezo wa kuzuia na kukabiliana na majanga katika sekta ya usafirishaji.

Azimio hilo linasema, washiriki wa mkutano huo, wamepokea kwa mikono miwili, wazo la Rais wa China Xi Jinping la kuanzishwa kwa Kituo cha kimataifa cha Uvumbuzi na Ujuzi kuhusu Usafirishaji Endelevu nchini China, kwamba kitatoa mchango katika maendeleo ya usafirishaji duniani na kujenga uwezo katika nchi zinazoendelea juu ya usafirishaji endelevu.

Akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya kufungwa kwa mkutano huo, Waziri wa Usafirishaji wa China Li Xiaopeng amesema kwamba, azimio hilo linaonesha matumaini kuhusu maendeleo ya usafirishaji endelevu duniani katika siku zijazo na linaweka hatua za utekelezaji wa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji.

 

Mawaziri wa usafirishaji, wataalam na vikundi vya kijamii vimeshiriki kwa njia ya mtandao na nje ya mtandao kwenye mkutano huo wa siku tatu, wakibadilishana mawazo na uzoefu katika maeneo kama vile shughuli za maisha ya watu, maendeleo kwa njia isiyoleta uchafuzi, juhudi za kupambana na janga la UVIKIO-19 na ufufukaji wa uchumi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha