Idadi ya watu waliokufa katika shambulio la watu wenye silaha Nigeria yafikia 43

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 19, 2021

LAGOS, Oktoba 18 (Xinhua) - Idadi ya waliokufa kutokana na shambulio la watu wenye silaha katika mji ulioko Kaskazini Magharibi mwa jimbo la Sokoto nchini Nigeria imefikia watu 43 kufuatia miili zaidi ikigunduliwa.

Aminu Waziri Tambuwal, gavana wa Jimbo la Sokoto, amesema katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni kwamba kundi la majambazi lilishambulia katika mji wa Goronyo Jumapili usiku na kuwaua watu wasiopungua 43.

Katika taarifa ya mapema siku hiyo, gavana alitaja idadi ya vifo kuwa karibu watu 30 kufuatia shambulio la watu hao wenye silaha.

"Hivi punde tumemaliza kikao na wadau wengine na nimethibitisha kwamba kwa bahati mbaya tumepoteza watu 43 kwenye tukio hilo," Tambuwal amesema katika taarifa hiyo iliyohuishwa.

Gavana huyo ametoa mwito wa kupeleka vikosi zaidi vya usalama katika jimbo hilo na kupelekwa kwa rasilimali zaidi kushughulikia changamoto za usalama.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari katika taarifa Jumatatu amelaani shambulio hilo, akisema siku za waliohusika "zinahesabika".

Huku akitoa wito kwa raia kuwa wavumilivu wakati jeshi linapanga mikakati ya jinsi ya kutoa pigo kubwa kwa wahalifu hao, rais amesema anaamini wahalifu wanaishi katika mahali pa ujinga wa kutoshindwa.

Kumekuwa na mfululizo wa mashambulizi ya watu wenye silaha nchini Nigeria katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha vifo na utekaji nyara.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha