Msemaji wa China akanusha tuhuma za Marekani dhidi ya Xinjiang

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 20, 2021

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya China Zhao Lijian Jumatatu ya wiki hii amesema nchi ya Marekani iliyo na hali mbaya ya haki za binadamu haifai kuwa "mtetezi wa haki za binadamu"

"Kuibua 'suala la haki za binadamu Xinjiang' ni njama ya wazi ya kisiasa, ambao lengo lake ni kudhoofisha ustawi na utulivu wa Xinjiang na kukwamisha maendeleo ya China" Msemaji Zhao amesema katika mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu swali kuhusu kauli ya Rais wa Marekani Joe Biden juu ya Xinjiang, mkoa unaojiendesha wa China.

Huku akibainisha kuwa Xinjiang ni mahali penye utulivu wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi, mshikamano wa makabila mbalimbali, watu wenye imani tofauti wanaishi kwa masikilizano, na watu wa Xinjiang wa makabila mbalimbali wanafurahia maisha ya furaha na haki zao halali zinazingatiwa kikamilifu, Zhao amesema kuwa kile kinachoitwa "ukandamizaji" na "kulazimishwa kufanya kazi" watu wa jamii ya Uygur huko Xinjiang ni uongo wa dhahiri.

"Marekani inajidai kuwa mlinzi wa demokrasia na haki za binadamu, lakini hali yake imekuwa mbaya sana," amesema.

Kwa mujibu wa Zhao, zaidi ya Wamarekani 700,000 wamekufa kwa janga la UVIKO-19 kutokana na Serikali ya Marekani kushindwa kuchukua hatua sahihi, na Marekani imeanzisha vita bila msingi wowote, kuua raia katika nchi zingine, na kusababisha majanga ya kibinadamu kwa kuwekea vikwazo kwa nchi mbalimbali bila kushirikisha pande zingine duniani.

Ameongeza kuwa, ukweli umethibitisha mara kwa mara kwamba Marekani inayojidai kuwa "Mnara wa demokrasia" imeanguka, na nchi hiyo haina sifa ya kuwa "mtetezi wa haki za binadamu", bado inaendelea kufanya hivyo kama "mhubiri mwenye kiburi"

"Marekani inapaswa kuangalia kwa kina hali yake mbaya ya haki za binadamu, ijishughulishe na mambo yake, na kuacha kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine na kudhoofisha masilahi ya nchi hizo kwa kisingizio cha haki za binadamu," Zhao amesema zaidi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha