Uganda yapokea shehena ya pili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 iliyotolewa na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 21, 2021
Uganda yapokea shehena ya pili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 iliyotolewa na China

KAMPALA - Uganda Jumanne ya wiki hii imepokea shehena ya pili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 aina ya Sinovac iliyotolewa na Serikali ya China.

Margaret Muhanga, waziri wa serikali wa huduma ya msingi ya afya, amepokea chanjo hizo katika Bohari Kuu ya Kitaifa ya Matibabu huko Entebbe, kilomita 40 Kusini mwa mji mkuu Kampala.

Amepongeza msaada huo kwa kuwa nchi yake imepanua kampeni yake ya utoaji wa chanjo na kufufua uchumi.

"Kwa kweli ni siku ya furaha kwetu kwa sababu tunapokea dozi zaidi za chanjo ya Sinovac, ambazo zitatusaidia kutoa chanjo kwa idadi kubwa ya watu, ili tuweze kufufua uchumi wetu kikamilifu," waziri amesema.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchni Uganda Zhang Lizhong, amesema msaada huo umekuja wakati ambao nchi hizo mbili zinasherehekea maadhimisho ya miaka 59 tangu nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na ni sehemu ya kujitolea kwa China kujenga jumuiya ya kimataifa yenye mustakabali wa pamoja wa afya.

Mbali na kuchangia dola za kimarekani milioni 100 kwenye mpango wa COVAX , China imeahidi kutoa dozi za ziada za chanjo milioni 100 mwaka huu kwa nchi nyingine zinazoendelea.

Yonas Tegegn Woldemariam, mwakilishi wa nchi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Uganda, pia amesifu msaada huo, akisema, "Kila dozi ya chanjo inayokuja Afrika inaokoa maisha na ikiwa tunaokoa maisha na tunatoa chanjo kwa watu wengi kadiri tuwezavyo na kuhakikisha utoaji wa chanjo kwa usawa, tunaweza kulishinda janga hilo"

Uganda ilipokea shehena ya kwanza ya chanjo za Sinovac mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya, hadi kufikia Jumapili ya wiki iliyopita, karibu dozi milioni 2.6 zilikuwa zimeshatolewa kwa raia wa Uganda.

Tangu Mwezi Machi mwaka jana, Uganda imeripoti jumla ya kesi 125,283 za UVIKO-19, watu 96,397 kati yao wamepona na watu wapatao 3,187 wamepoteza maisha.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha