Marekani bado iko tayari kuzungumza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK): Ikulu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 21, 2021

WASHINGTON - Ikulu ya Marekani imesema mapema wiki hii kwamba Marekani bado imejiandaa kuzungumza na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) baada ya jaribio lake la kurusha makombora hivi karibuni.

Wakuu wa Majeshi ya pamoja ya Korea Kusini (JCS) wamesema Jumanne ya wiki hii kwamba DPRK ilirusha kombora la masafa mafupi katika eneo la bahari la mashariki. Shirika la Habari la DPRK (KCNA) limesema mapema Jumatano kwa saa za huko kwamba nchi hiyo imefanya jaribio la kurusha makombora chini ya maji.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki amewaambia waandishi wa habari kwamba Marekani inalaani urushaji wa makombora huku akisema "urushaji huu pia unasisitiza hitaji la haraka la mazungumzo na diplomasia."

"Ahadi yetu ni kwamba tunaweza kukutana mahali popote, wakati wowote bila sharti lolote. Pia tunajadiliana kwa karibu na washirika wetu kuhusu jambo hilo," ameongeza. "Tuko tayari kushirikiana na DPRK kwa njia ya kidiplomasia."

Aidha, Jumanne ya wiki hii, Mwakilishi Maalum wa Marekani nchini DPRK Sung Kim alifanya mkutano wa pande tatu na wenzake kutoka Korea Kusini na Japani juu ya hali ya sasa kwenye Peninsula ya Korea, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

"Kim amesisitiza kuwa Marekani inalaani urushaji wa makombora la DPRK uliofanywa tarehe 9 Oktoba, ambalo linakiuka maazimio mengi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na ameitaka DPRK kuacha uchochezi zaidi na kushiriki katika mazungumzo endelevu na ya kimsingi" imesema taarifa hiyo.

Serikali ya Marekani imependekeza mara kadhaa kwamba inataka kushiriki mazungumzo na DPRK juu ya suala la kuifanya Peninsula ya Korea iwe eneo lisilo na silaha za nyuklia lakini haijaonesha nia yake ya kupunguza vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Kiongozi mkuu wa DPRK Kim Jong Un amesema wiki iliyopita kwamba hakujakuwa na "msingi wowote wa kivitendo" kwa kuamini ishara ya hivi karibuni ya Marekani kwamba Marekani haina uhasama dhidi ya Pyongyang, akiilaumu Korea Kusini kwa "vigezo viwili" vya kuendelea kujenga uwezo wa kijeshi.

Hata hivyo Kim alibainisha kuwa adui wa DPRK ni "vita yenyewe, sio nchi au vikosi kama Korea Kusini na Marekani."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha