Tanzania yashuhudia kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI na vifo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 02, 2021

DAR ES SALAAM - Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa taarifa akisema kuwa maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI yamepungua kwa asilimia 38.2 kutoka 110,000 ya Mwaka 2010 hadi 68,000 ya Mwaka wa 2020.

Katika hotuba yake ya kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani mkoani Mbeya, Majaliwa amesema vifo vinavyotokana na VVU/UKIMWI nchini Tanzania vimepungua kwa nusu kutoka vifo 64,000 Mwaka 2010 hadi vifo 32,000 mwaka 2020.

Majaliwa amesema mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na ugonjwa huo yametokana na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine muhimu.

Amesema upimaji wa VVU/UKIMWI nao uliongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 83 mwaka 2019.

Majaliwa ameongeza kuwa matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU/UKIWMI yaliongezeka kwa asilimia 92 mwaka 2019 kutoka asilimia 87 ya mwaka 2016.

Amesema Serikali pia imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma za wakina mama na watoto ambazo zimesaidia kupunguza kasi ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa watoto wanaozaliwa kutoka asilimia 18 hadi 7.

Hata hivyo, awali wakati akimkaribisha Waziri Mkuu Majaliwa kutoa hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Ajira, Uratibu na Bunge Jenista Mhagama alisema kwamba, pamoja na kupungua kwa maambukizi mapya, maambukizi hayo mapya ya VVU/UKIMWI kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 yamezidi kuongezeka huku wasichana wakiongoza.

Kupitia ripoti mbalimbali za vyombo vya habari nchini Tanzania, Mhagama amenukuliwa akisema kwamba, taarifa za utafiti zinaonesha kwamba maambikizi mapya ya VVU/UKIWMI yanawakabili vijana wengi zaidi wenye umri huo na kwamba yamefikia asilimia 40 huku zaidi ya asilimia 80 kati yao ni wa kike jambo ambalo alieleza ni hatari kwa nguvu kazi ya taifa hilo la Afrika Mashariki. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha