China yasema Makubaliano kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika yamefikiwa katika mkutano wa FOCAC

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 02, 2021
China yasema Makubaliano kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika yamefikiwa katika mkutano wa FOCAC
Mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo ya mradi wa kuzalisha umeme wa De Aar uliyowekezwa na Kampuni ya Umeme ya Longyuan ya China na washirika wake wa Afrika Kusini huko De Aar, Afrika Kusini. Picha imepigwa Novemba 22, 2021 (Xinhua/Lyu Tianran)

DAKAR – Mjumbe wa Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kuwa China na Afrika zimefikia makubaliano muhimu kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Wang amesema hayo Jumanne ya wiki hii katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal Aissata Tall Sall na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mkutano huo.

Wang Yi amebainisha makubaliano kati ya China na Afrika katika mkutano huo kama ifuatavyo:

Kwanza, pande zote mbili zimekubaliana kuhimiza moyo wa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika. Dhamira hiyo ilipendekezwa na Rais Xi Jinping wa China kwa mara ya kwanza katika hotuba yake ya ufunguzi huo. Imekubalika kwamba, bila kujali jinsi hali ya kimataifa inaweza kubadilika na matatizo na vikwazo gani China na Afrika zitakabiliana navyo, pande hizo mbili zitaendelea kuwa na nia ya dhati ya kuimarisha uaminifu wa kisiasa na kuzidisha ushirikiano wa kivitendo ili moyo wa urafiki na ushirikiano kati ya pande hizo mbili uendelezwe na kurithishwa kizazi baada ya kizazi.

Pili, China na Afrika zitafanya kazi pamoja ili kulishinda janga la UVIKO-19. Akihutubia ufunguzi wa mkutano huo, Rais Xi alitangaza kwa dhati kwamba China itatoa dozi za ziada za chanjo dhidi ya UVIKO-19 bilioni 1 kwa Afrika ili kusaidia Umoja wa Afrika kufikia lengo lake la kuchanja asilimia 60 ya watu wa Afrika ifikapo Mwaka 2022.

Tatu, pande zote mbili zitafanya jitihada kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika. Katika mkutano huo, Xi ametangaza kuwa, China itatekeleza mipango tisa pamoja na nchi za Afrika, ambayo ni tangazo lenye nguvu la China kuendelea kujitolea kwa Afrika na kudumisha mwelekeo wa ushirikiano kati ya China na Afrika.

Nne, pande hizo mbili zitafanya kazi pamoja ili kutekeleza diplomasia ya pande nyingi. China na Afrika zitaendelea kuungana mkono kithabiti katika masuala kuhusu masilahi ya kimsingi na mambo yanayofuatiliwa, kulinda kwa pamoja mfumo wa kimataifa ambao Umoja wa Mataifa ni msingi wake na utaratibu wa kimataifa wenye msingi wa sheria za kimataifa, na kuongeza uwakilishi na sauti ya nchi zinazoendelea kwenye masuala ya kimataifa.

Pande hizo mbili zimekubaliana kwamba zitapinga kwa uthabiti vikwazo vyovyote vya upande mmoja, uingiliaji kati wa mambo ya ndani ya nchi nyingine na ubaguzi wa rangi, na zitakuza maadili ya pamoja ya binadamu ya amani, maendeleo, usawa, haki, demokrasia na uhuru, ili kutoa mchango mkubwa zaidi katika kulinda usawa na haki Duniani.

Tano, China na Afrika zitajenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja ya pande hizo mbili katika zama mpya. Makubaliano hayo yanasema, China inashukuru nchi za Afrika kwa kukaribisha na kuunga mkono Mpango wa Maendeleo ya Kimataifa uliopendekezwa na Rais Xi.

Makubaliano hayo yanaeleza kuwa, China iko tayari kutembea na nchi za Afrika bega kwa bega katika njia ya maendeleo na ustawi, na kujenga kwa pamoja jumuiya yenye mustakabali wa pamoja ya China na Afrika katika zama mpya. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha