Maafisa wa kijeshi wa Somalia na AU wanoa ujuzi wa kukusanya taarifa za kijasusi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2021

MOGADISHU - Wanajeshi 20 kutoka Jeshi la ulinzi wa Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) wamehitimu mafunzo yao ya siku nne yenye lengo la kuimarisha ujuzi wa kukusanya taarifa za kijasusi ambazo ni muhimu kwa kupunguza nguvu za Kundi la kigaidi la al- Shabab nchini humo.

Ujumbe wa AU umesema Jumapili kwamba mafunzo hayo ya kukusanya na kubadilishana taarifa yanasaidia kuimarisha ushirikiano katika kuendesha operesheni za pamoja za kijeshi dhidi ya magaidi nchini Somalia.

Kamanda wa Kikosi cha AMISOM Diomede Ndegeya amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa operesheni za kijeshi, akibainisha kuwa ujasusi au taarifa ni uwezo muhimu katika operesheni za kijeshi, na muhimu kwa AMISOM na SNA.

"Kwa kutumia taarifa kwa ufanisi, tunaweza kumchambua adui na kufichua nia yake, huku tukisaidia kulinda na kuunga mkono vikosi vyetu," Ndegeya amesema katika taarifa iliyotolewa mjini Mogadishu, Mji Mkuu wa Somalia.

Ndegeya amesema kuwa ujasusi unaweza kuongeza upangaji wa operesheni na kufanya maamuzi, akibainisha kuwa hali nchini Somalia ni ngumu na inabadilika kila mara, na hivyo kuhitaji ufahamu mzuri wa hali halisi.

Ndegeya amewataka washiriki hao kuhamisha uelewa na ujuzi walioupata katika mafunzo hayo kwenda kwenye kazi zao katika vitengo vyao, ili kuwezesha ujumbe huo kufikia majukumu yake hasa katika juhudi za kupunguza nguvu za Kundi la al-Shabaab na kurejesha amani na utulivu nchini Somalia.

Kozi ya msingi ya J2 ilihudhuriwa na maafisa saba wa jeshi la SNA na 13 wa AMISOM.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha