Russia yasema jeshi la anga la Marekani linatishia usafiri wa anga wa abiria

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2021

MOSCOW – Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova amesema kwamba vitendo hatari vya Jeshi la Anga la Marekani vimezua tishio kwa usafiri wa anga wa abiria nchini humo.

Kupitia chapisho lake la telegramu Jumapili ya wiki iliyopita, Zakharova ameelezea wasiwasi wake juu ya ongezeko la kasi la safari za ndege za Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi (NATO) karibu na mpaka wa Russia pamoja na anga la Bahari Nyeusi.

Amesema kuwa siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, ndege ya uchunguzi ya Marekani ya aina ya CL 600 ilishuka kutoka mita 11,000 hadi 9,200 juu ya Bahari Nyeusi, karibu na eneo la uwajibikaji wa udhibiti wa usafiri wa anga la Russia, na kuvuruga njia za ndege mbili za abiria.

Zakharova amesisitiza kwamba, wafanyakazi wa ndege hiyo hawakujibu maombi ya mara kwa mara kutoka kwa mamlaka za udhibiti safari za anga la Russia.

Amebainisha kwamba, waongoza safari za anga wa Russia walihakikisha usalama wa ndege za abiria kwa kubadilisha mara moja mwelekeo na urefu wa wima wa masafa ya ndege.

"Ingawa sasa janga limeepukwa katika anga la juu ya Bahari Nyeusi, hii haimaanishi kuwa Marekani na NATO zinaweza kuweka maisha ya watu hatarini bila hatua kuchukuliwa" ameandika Zakharova, huku akibainisha kuwa mamlaka ya anga ya Russia itatoa malalamiko rasmi kupitia njia za kidiplomasia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha