Zambia yapokea shehena ya pili ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 25, 2022

Waziri wa Afya wa Zambia Sylvia Masebo (wa pili kutoka kushoto, mbele) na Balozi wa China nchini Zambia Li Jie (wa kwanza kulia, mbele) wakihudhuria hafla ya kuwasili kwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na China kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda mjini Lusaka, Zambia, Januari 24, 2022. Zambia siku ya Jumatatu ya wiki hii imepokea shehena mpya ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali ya China. (Picha na Martin Mbangweta/Xinhua)

LUSAKA - Zambia Jumatatu ya wiki hii imepokea shehena mpya ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali ya China.

Dozi 400,000 za chanjo hizo zilipokelewa na Li Jie, Balozi wa China nchini Zambia na Sylvia Masebo, Waziri wa Afya wa Zambia, wakati wa hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda mjini Lusaka, mji mkuu wa nchi hiyo.

Akihutubia kwenye hafla hiyo, balozi Li Jie alisema serikali za nchi hizo mbili zimekubaliana kwamba chanjo milioni moja ambazo mwaka jana China iliahidi kutoa zitatumwa kwa awamu tatu.

Amesema kwamba, China iko tayari kukusanya rasilimali nyingi zaidi kusaidia Zambia kukabiliana na janga la UVIKO-19 ili kuthibitisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili kwa miaka mingi.

Ameongeza kwamba, mchango wa sasa ni nyongeza kwenye dozi nyingine 100,000 zilizotolewa mwaka jana.

Kwa mujibu wake, nchi hizo mbili zimeshirikiana katika mapambano dhidi ya janga hilo tangu kisa cha kwanza cha UVIKO-19 kilipotangazwa katika nchi hiyo mnamo Machi 2020, na ameishukuru Zambia kwa msaada iliotoa wakati China iliporekodi maambukizi ya kwanza ya virusi vya korona Mwaka 2019.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Zambia ameishukuru China kwa mchango huo, akisema msaada huo ni alama ya uhusiano wa kindugu uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Waziri huyo amesema chanjo hizo zimekuja wakati muafaka ambapo nchi hiyo imeanza kutoa dozi za nyongeza za chanjo pamoja na kuanzishwa kwa zoezi la utoaji chanjo kwa watoto wenye umri wa miaka 12 na zaidi.

Waziri huyo amesema, Serikalil ya Zambia imelenga kuchanja takriban asilimia 70 ya watu wanaostahili kuchanjwa kufikia Juni mwaka huu.

Amesema urafiki kati ya nchi hizo mbili umejikita kwa watu licha ya mabadiliko ya serikali, na kuongeza kuwa dhamira ya serikali ya sasa ni kuendelea kujenga uhusiano wa kirafiki uliowekwa na viongozi waasisi wa nchi hizo mbili.

Masebo amesema Serikali ya Zambia inaishukuru China kwa misaada ambayo imekuwa ikitoa kwa miaka mingi katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya afya na maendeleo ya miundombinu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha