Zaidi ya watoto milioni 10 nchini Marekani wameambukizwa UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 26, 2022

Wanafunzi wakihudhuria darasa la ana kwa ana katika moja ya shule huko Los Angeles, California, Marekani, Aprili 13, 2021. (Xinhua)

WASHINGTON - Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Chuo cha Madaktari wa Watoto cha Marekani (AAP) na Chama cha Hospitali ya Watoto, zaidi ya watoto milioni 10 nchini Marekani wamepatikana na virusi vya UVIKO-19 tangu kuanza kwa janga hilo.

Ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatatu jioni ya wiki hii inaeleza kwamba, jumla ya watoto 10,603,034 walioambukizwa UVIKO-19 wameripotiwa kote nchini Marekani kufikia Januari 20 mwaka huu, na maambukizi ya watoto yalichukua asilimia 18.4 ya visa vyote vilivyothibitishwa,

Visa vya UVIKO-19 miongoni mwa watoto vimeongezeka sana kote Marekani wakati wa kuongezeka kwa maambukizi yaliyosababishwa na kirusi cha korona aina ya Omicron.

Kwa mujibu wa AAP, zaidi ya visa vya maambukizi ya UVIKO-19 kwa watoto milioni 1.1 viliripotiwa katika wiki iliyopita, ikiwa ni karibu mara tano ya kiwango cha kilele cha ongezeko la maambukizi wakati wa majira ya baridi mwaka jana.

AAP imeeleza kwamba, idadi hii ilikuwa ongezeko la asilimia 17 zaidi kwenye visa 981,000 vilivyorekodiwa wiki moja kabla na kuongezeka maradufu kwa maambukizi ya virusi vya korona kutoka wiki mbili zilizopita.

Zaidi ya visa vya maambukizi ya UVIKO-19 kwa watoto milioni 2 vimerekodiwa katika wiki mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa AAP, hali hiyo inawakilisha wiki ya 24 mfululizo kwa visa vya maambukizi ya UVIKO-19 kwa watoto nchini Marekani kuendelea kuwa zaidi ya 100,000. Tangu wiki ya kwanza ya Septemba, 2021 kumekuwa na zaidi ya visa milioni 5.6 vya ziada vya UVIKO-19 kwa watoto. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha