UNICEF yazindua kampeni ya kuongeza utoaji chanjo dhidi ya UVIKO-19 barani Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 27, 2022

NAIROBI - Mfuko wa kuhudumia watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) siku ya Jumatano wiki hii umeanza kampeni ya wiki nane ya kusaidia kuongeza ugawaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 kote barani Afrika.

UNICEF imesema ripoti ya kwanza kutoka mfumo wa mawasiliano wa vijana mtandaoni (U-Report Challenge) ambayo inakuja wiki moja baada ya COVAX kuwasilisha dozi bilioni moja nchini Rwanda, inatoa wito kwa washiriki wa U-Report wapatao milioni 13.3 barani Afrika kusaidia kupata chanjo kwa wale ambao hawajachanjwa.

"Kupitia kuboresha ufikiaji na imani katika chanjo dhidi UVIKO-19, changamoto ya #GiveItAShot inalenga kuamsha ari ya vijana katika kuwahamasisha wale wanaofaa kuchanjwa katika jumuiya zao kupata chanjo," inasema UNICEF katika taarifa iliyotolewa katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.

U-Report ni chombo cha kutuma ujumbe ambacho huwawezesha vijana duniani kote kujihusisha na kuzungumza kuhusu masuala ambayo ni muhimu kwao.

U-Report kwa sasa inafanya kazi katika nchi 88 duniani kote, ikiwa na washiriki milioni 19.3 kote duniani, na inafanya kazi kupitia SMS, Facebook Messenger, Viber, Telegram, na WhatsApp.

Kwa mujibu wa UNICEF, taarifa na ujumbe wa uhamasishaji kuhusu UVIKO-19 umeandaliwa na kusambazwa kupitia SMS, Facebook Messenger na njia nyinginezo za mawasiliano.

UNICEF imesema kampeni hiyo iliyopewa jina la "U-Report #GiveItAshot Challenge" ambayo mwanzoni italenga nchi sita za bara hilo ambazo ni Cote d'Ivoire, Ghana, Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, na Zimbabwe itafanyika kwa wiki nane.

Imesema jumbe za kila wiki zitatumwa kwenye U-Report kuhimiza vijana kujifunza kuhusu chanjo dhidi ya UVIKO-19. Vijana hao watashiriki katika shughuli za kijamii (mtandaoni na nje ya mtandao).

Kwa mujibu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa (Africa CDC), inakadiria kuwa takriban asilimia 10 ya watu wazima katika bara la Afrika wamechanjwa. Jumla ya idadi ya maambukizi ya virusi vya korona barani humo ilifikia 10,609,112 kufikia Jumanne ya wiki hii.

Taarifa inasema idadi ya vifo vinavyohusiana na UVIKO-19 katika bara zima ni 237,197 na wagonjwa 9,534,559 wamepona hadi sasa. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha