Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Tonga wazungumza kwa simu kuhusu msaada wa dharura baada ya milipuko ya volkano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 27, 2022

Baadhi ya wakazi nchini Tonga wakisafisha majivu na vifusi katika barabara ya Nuku'alofa, Mji Mkuu wa Tonga. (Picha na Marian Kupu/Xinhua)

BEIJING – Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi Jumatano ya wiki hii amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ufalme wa Tonga, Fekitamoeloa Katoa 'Utoikamanu, kuhusu milipuko ya hivi majuzi ya volkano.

Wang amesema tangu volcano hiyo ilipolipuka huko Tonga mnamo Januari 15, Serikali ya China imezingatia sana na watu wa China wamewahurumia watu wa Tonga.

Amesema kwamba, Rais wa China Xi Jinping mara moja alituma ujumbe wa masikitiko na pole kwa Mfalme wa Tonga, na China ikapeleka misaada haraka Tonga, na kuwa moja ya nchi za kwanza duniani kutoa msaada kwa nchi hiyo ya Kisiwa cha Bahari ya Pasifiki ya Kusini.

Kama rafiki mzuri na mshirika wa Tonga, China iko tayari kusimama kidete na watu wa Tonga katika wakati huu mgumu, amesema Wang Yi na kuongeza kuwa, vifaa vya dharura vilivyonunuliwa na China huko Fiji vitawasili Tonga Alhamisi (leo), na misaada zaidi kutoka China iko njiani.

Wang Yi amesema kwamba, China imetenga mahitaji na vifaa vya misaada kwa nchi kulingana na mahitaji ya Tonga, kama vile maji ya kunywa, chakula, jenereta, pampu za maji, vifaa vya huduma ya kwanza, nyumba za muda na matrekta.

Amesema, baadhi ya vifaa vya msaada vitasafirishwa na ndege za kijeshi za China na kuwasili Alhamisi (leo) asubuhi, wakati vingine vitasafirishwa na meli za kivita za China. Amebainisha kuwa, pande hizo mbili zinapaswa kurahisisha taratibu za makabidhiano na kupeleka misaada hiyo katika maeneo yenye uhitaji zaidi ya nchini Tonga kwa wakati.

Kwa upande wake, 'Utoikamanu amesema kuwa China iliitikia mara moja na ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kutoa msaada wa dharura na maafa kwa Tonga baada ya volkano hiyo kulipuka siku 11 zilizopita.

Ametoa shukrani za dhati kwa China kwa msaada wake kwa niaba ya Serikali na watu wa Tonga.

Meli iliyobeba msaada wa dharura kutoka China hadi Tonga ikiwa tayari kuanza safari katika Bandari ya Suva's Walu Bay, Fiji, Januari 24, 2022. (Xinhua/Zhang Yongxing)

Meli iliyobeba msaada wa dharura kutoka China hadi Tonga ikianza safari kwenye Bandari ya Suva's Walu Bay, Fiji, Januari 24, 2022. (Xinhua/Zhang Yongxing)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha