Waziri Mkuu wa Uingereza agoma kujiuzulu katikati ya tuhuma za kukiuka hatua za kudhibiti UVIKO-19

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 27, 2022
Waziri Mkuu wa Uingereza agoma kujiuzulu katikati ya tuhuma za kukiuka hatua za kudhibiti UVIKO-19
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akiondoka ofisini kwake Mtaa wa 10 wa Downing kwa ajili ya Kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu bungeni mjini London, Uingereza, Januari 12, 2022. (Picha na Tim Ireland/Xinhua)

LONDON - Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson Jumatano amegomea wito wa kumtaka kujiuzulu wakati matokeo ya uchunguzi rasmi kuhusu sherehe zinazodaiwa kufanyika kwenye ofisi yake katika eneo la Whitehall na Mtaa wa Downing miaka miwili iliyopita kinyume na hatua zilizokuwa zimewekwa na serikali kukabiliana na maambukizi ya virusi vya korona yakikaribia kutolewa.

Katika kikao cha kila wiki cha Maswali kwa Waziri Mkuu (PMQs) kwenye Bunge la Chini la Uingereza (House of Commons), Johnson amekataa kujiuzulu huku viongozi wa vyama vya upinzani wakimtaka afanye hivyo.

Alipoulizwa na Kiongozi wa Chama Kikuu cha upinzani cha Labour Keir Starmer, ikiwa anapaswa kujiuzulu kwa kubadilisha maelezo yake kuhusu mikusanyiko (ya sherehe hizo) na kulipotosha Bunge, Johnson amesema "Hapana."

Wakati Kiongozi wa Chama cha Taifa cha Scotland (SNP) Ian Blackford, alipomuuliza Johnson ni lini ataelewa uhalisia na kujiuzulu, Johnson alijibu kuwa hana nia kabisa ya kufanya kile anachopendekeza kiongozi huyo.

Kufichuliwa kwa msururu wa sherehe hizo zinazoelezwa kukiuka hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya korona, kumekasirisha umma wa Uingereza, ambao ulifuata kwa utii hatua za kujitenga kijamii zilizowekwa na serikali, ambazo ziliwazuia kukutana na marafiki na familia kwa miezi mingi ya mwaka 2020 na 2021. Familia kadhaa zilishindwa hata kuwaaga ndugu waliofariki au kuhudhuria mazishi.

Wiki mbili zilizopita, Johnson aliomba msamaha kwa kuhudhuria karamu kwenye bustani ya Mtaa wa Downing iliyofanyika Mei 20, 2020, wakati wa utekelezaji wa hatua za kwanza za kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 nchini humo. Alidai kwamba, aliamini sherehe hiyo ilikuwa ni tukio la kikazi na alikaa hapo kwa dakika 25 tu.

Jumatatu wiki hii, Kituo cha Televisheni cha ITV nchini Uingereza kiliripoti kuwa Johnson alihudhuria pia sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika Juni 19, 2020, katika Mtaa wa Downing, ambayo ilihudhuriwa na karibu watu 30 licha ya marufuku ya mikusanyiko ya kijamii ya ndani.

Bado haijafahamika ni lini ripoti hiyo inayoandaliwa na Sue Gray, mtumishi mkuu wa serikali aliyepewa jukumu la kuchunguza wahusika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, itatolewa. Kabla ya maswali kwa waziri mkuu bungeni jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Liz Truss amesema serikali bado haijapokea matokeo ya ripoti ya Grey, lakini amesema kwamba itatolewa hivi karibuni.

Siku ya Jumanne wiki hii, Jeshi la Polisi la Jiji la London lilitangaza kuanza kwa uchunguzi wa matukio kadhaa ambayo yalifanyika Mtaa wa Downing na Whitehall katika miaka miwili iliyopita kuhusiana na uwezekano wa ukiukaji wa hatua za kudhibiti UVIKO-19, likitoa sababu ya "ufuatiliaji mkubwa wa umma" wa suala hilo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha