Mwanadiplomasia Mwandamizi wa China afanya mazungumzo kwa njia ya simu na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 19, 2022

BEIJING - Yang Jiechi, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Jumatano wiki hii amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan.

Yang, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, amesema nchi hizo mbili zinapaswa kutekeleza kwa dhati maafikiano muhimu yaliyofikiwa kati ya Rais Xi Jinping wa China na Rais Joe Biden wa Marekani kuhusu uhusiano baina ya China na Marekani.

Yang amesema, hivi karibuni, pande hizo mbili zimefanya majadiliano kuhusu majeshi ya nchi hizi mbili, mabadiliko ya tabianchi, afya na kilimo, ambayo yamekuwa yenye manufaa, na mwelekeo wa mazungumzo unapaswa kudumishwa.

“Wakati huo huo, ni lazima ifahamike kwamba kwa muda sasa, Marekani imekuwa ikichukua mfululizo wa maneno na vitendo visivyo sahihi vinavyoingilia mambo ya ndani ya China na kudhuru maslahi ya China, jambo ambalo China inapinga vikali na imejibu kwa nguvu” Yang amesema.

Amesema kwamba, Marekani lazima ioanishe maneno na vitendo vyake, kutafsiri ahadi zake katika sera na vitendo halisi, kushirikiana na China, kudhibiti ipasavyo tofauti kati ya pande hizo mbili, na kufanya mambo ya kiujenzi ili kurejesha uhusiano wa pande hizo mbili kwenye njia ya maendeleo ya utulivu kwa hatua madhiubutio .

“Suala la Taiwan ni muhimu zaidi, nyeti na la msingi zaidi katika uhusiano wa China na Marekani” amesisitiza Yang, huku akiongeza kuwa upande wa Marekani umeweka wazi mara nyingi kwamba unafuata sera ya Kuwepo kwa China moja na hauungi mkono "Taiwan ijitenge na China ".

“Hata hivyo, hatua na kauli za hivi karibuni za Marekani kuhusu suala la Taiwan ni tofauti kabisa” amesema Yang, akibainisha kwamba ikiwa upande wa Marekani utaendelea kucheza " karata ya Taiwan" na kwenda zaidi kwenye njia mbaya, bila shaka itaweka hali katika hatari kubwa.

“China inaitaka Marekani kutambua na kukubali uhalisia wa hali, kuheshimu kikamilifu ahadi zake na kufuata kanuni ya kuwepo kwa China moja na masharti ya nyaraka tatu za pamoja za China na Marekani”, amesema Yang, akisisitiza kuwa upande wa China utachukua hatua thabiti kulinda mamlaka yake ya nchi na maslahi ya usalama, na upande wa Marekani unaweza kutegemea China kutimiza ahadi yake.

Yang amesema, kutafuta amani, ushirikiano na maendeleo ni mwelekeo wa jumla wa eneo la Asia na Pasifiki na vilevile ni matarajio ya pamoja ya watu.

Viongozi hao wawili, pia wamebadilishana maoni kuhusu hali ya mgogoro wa Ukraine, Peninsula ya Korea na masuala mengine ya kimataifa na kikanda. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha