WHO yaidhinisha chanjo ya tatu dhidi ya UVIKO-19 kutoka China kwa matumizi ya dharura

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2022

Picha iliyopigwa Machi 30, 2021 ikionyesha mwonekano wa nje wa makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Geneva, Uswisi. (Xinhua/Chen Junxia)

GENEVA - Shirika la Afya Duniani (WHO) Alhamisi wiki hii limeidhinisha chanjo dhidi ya UVIKO-19 aina ya CONVIDECIA iliyotengenezwa na kampuni ya dawa kutoka China ya CanSino Biologics kwa matumizi ya dharura, na kuifanya kuwa chanjo ya tatu ya China baada ya Sinopharm na Sinopec kuthibitishwa na WHO kupitia Orodha ya Matumizi ya Dharura (EUL).

WHO imesema katika taarifa yake kwamba tathmini ya CONVIDECIA "imezingatia mapitio ya data kuhusu ubora, usalama, ufanisi, mpango wa udhibiti wa hatari, kufaa kwa programu yake na ukaguzi wa eneo la uzalishaji wake uliofanywa na WHO."

"Kundi la Ushauri wa Kiufundi kwa Orodha ya Matumizi ya Dharura, lililoundwa na WHO na linalohusisha wataalam wa udhibiti kutoka kote duniani, limeamua kuwa chanjo hiyo imefikia vigezo vya WHO vya kujikinga na UVIKO-19 na manufaa ya chanjo hiyo ni makubwa kuliko hatari," taarifa hiyo imesema.

CONVIDECIA, inayotolewa kwa dozi moja, "inatokana na virusi vya adeno vya binadamu vilivyorekebishwa ambavyo vinaonyesha protini ya S ya SARS-CoV-2," virusi vinavyosababisha UVIKO-19. Chanjo hiyo iligundulika kuwa na asilimia 64 ya ufanisi dhidi ya ugonjwa wenye kuonesha dalili kiasi na asilimia 92 dhidi ya UVIKO-19 wenye dalili kali.

CONVIDECIA pia imekaguliwa upya na Kundi la Ushauri wa Kimkakati la WHO la Wataalamu wa Chanjo (SAGE), ambalo linatunga sera na mapendekezo mahususi ya chanjo kwa matumizi ya umma. SAGE inapendekeza matumizi ya CONVIDECIA kwa dozi moja ya mililita 0.5 katika makundi yote ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi. Mapendekezo ya kina kuhusu matumizi ya chanjo hiyo yatatolewa hivi karibuni.

WHO iliidhinisha chanjo dhidi ya UVIKO-19 kutoka China za Sinopharm na Sinovac mwaka jana. 

Balozi wa China katika Jamhuri ya Kongo Ma Fulin (wa kwanza kulia) akikabidhi sanduku la chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa Ofisa wa Serikali ya Kongo kwenye uwanja wa ndege wa Maya-Maya huko Brazzaville, Jamhuri ya Kongo, Januari 20, 2022. (Xinhua)

Wafanyakazi wakibeba chanjo dhidi ya UVIKO-19 kutoka China kwenye uwanja wa ndege wa Managua, Nicaragua, Desemba 24, 2021. (Xinhua/Xin Yuewei)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha