Kansela Scholz wa Ujerumani asema hakuna njia za mkato kwa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2022

BERLIN - Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema siku ya Alhamisi wiki hii kwamba hakutakuwa na njia za mkato kwa ombi la Ukraine la kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU).

Scholz amesema katika hotuba yake kwa Bundestag, Baraza la chini la Bunge la Ujerumani kwamba, Kamisheni ya Ulaya inatarajiwa kukamilisha tathmini yake ya awali ya ombi la uanachama wa Ukraine katika EU mwishoni mwa Juni. “Kutoruhusu njia za mkato katika safari ya Ukraine ya kujiunga na EU, hata hivyo, ni ‘hitaji la usawa’ kuelekea kwa nchi nyingine za Balkan Magharibi” Scholz amesema.

Mchakato wa kujiunga na EU unaweza kuchukua miaka kadhaa. Nchi za Balkan Magharibi za Montenegro, Serbia, Albania na Macedonia Kaskazini zimekuwa zikitambuliwa kama nchi zilizoomba uanachama wa EU kwa kati ya miaka minane na 17.

Wiki iliyopita, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia alizima matumaini ya Ukraine ya kujiunga kwa haraka na Umoja wa Ulaya. "Sote tunajua vyema kwamba mchakato ambao utawaruhusu kujiunga utachukua miaka kadhaa, na uwezekano mkubwa ni kuchukua miongo kadhaa," alisema.

Kuelekea mkutano maalumu wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, Scholz amezungumza akiunga mkono mfuko wa mshikamano wa Ulaya kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine. "Tayari ni wazi, ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa, ufufuaji wa uchumi wa Ukraine, yote haya yatagharimu mabilioni ya fedha," amesema.

Mfuko wa mshikamano "utachangiwa na michango kutoka kwa EU na washirika wetu wa kimataifa," amesema, akisisitiza kwamba EU imebidi kuanza maandalizi sasa kuisaidia Ukraine kwenye "njia yake ya Ulaya."

Scholz amesisitiza kuwa mshikamano barani Ulaya pia unahitajika ili kukabiliana na ongezeko la bei ya nishati. "Katika ngazi ya Ulaya, suala kuu ni kuhakikisha kuwa hakuna vikwazo katika usambazaji wa nishati kwenye nchi wanachama."

“Ili kuepuka uhaba wa nishati, Ujerumani lazima ijitegemee kwa nishati ya mafuta na kupanua mitandao ya nishati inayovuka mipaka ndani ya nchi za Ulaya”, Scholz amesema, huku akisifu maendeleo yaliyofikiwa kwa pamoja na Denmark, Ubelgiji na Uholanzi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha