Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika chaonya uwezekano wa aina mpya ya virusi vya Korona

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Mei 20, 2022

ADDIS ABABA - Ahmed Ogwell, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC), ameonya kuwa kuna uwezekano kwamba aina mpya ya virusi vya Korona itaibuka barani Afrika katika siku zijazo.

"Ongezeko hilo ni ishara tosha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa aina mpya, ambayo inaweza kuambukiza zaidi," Ogwell amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana Alhamisi.

Kwa mujibu wa takwimu za kituo hicho, Bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la wastani wa asilimia 36 la visa vipya vya UVIKO-19 katika muda wa wiki nne zilizopita, huku nchi za Afrika ya Kati na Mashariki zikiripoti kuongezeka kwa maambukizi mapya ya UVIKO-19 kwa asilimia 113 na 54, mtawalia.

Kituo hicho kilicho chini ya Umoja wa Afrika, kimetoa wito wa kuongeza kasi ya upimaji ili kujua ni sehemu gani za bara hilo ambazo aina mpya za virusi vya Korona zinagunduliwa.

"Tunahitaji kufanya upimaji na mpangilio zaidi wa jeni ili tuweze kuelewa milipuko iko wapi na kutambua ni aina gani za virusi vinavyogunduliwa" Ogwell amesema.

Pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa utoaji wa chanjo ili kushughulikia kwa uendelevu changamoto ya kiwango cha chini cha utoaji wa chanjo dhidi ya janga hili katika bara zima. "Tunaona idadi ya vifo inayoongezeka kutokana na janga hili huku visa vikiongezeka katika wiki nne zilizopita."

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi huyo, nchi tano za Afrika zimeripoti idadi kubwa zaidi ya visa vipya vilivyothibitishwa vya UVIKO-19 katika wiki moja iliyopita huku Afrika Kusini ikiripoti visa 50,404, Tanzania 1,482, Namibia 1,054, Zimbabwe 910 na Burundi 817. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha