Nchi za Ulaya zarejea tena kutumia makaa ya mawe huku vikwazo dhidi ya nishati ya Russia vikirudi kuziathiri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 23, 2022
Nchi za Ulaya zarejea tena kutumia makaa ya mawe huku vikwazo dhidi ya nishati ya Russia vikirudi kuziathiri
Picha iliyopigwa Aprili 28, 2022 ikionyesha ofisi za kampuni kubwa ya nishati ya Gazprom ya Russia huko Moscow, Russia (Picha na Alexander Zemlianichenko Jr/Xinhua)

BERLIN - Nchi nyingi za Ulaya zinafikiria kurejea kwenye makaa ya mawe ili kuhakikisha usambazaji wa nishati huku usambazaji wa gesi kutoka Russia ukishuka kutokana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya katika wiki za hivi karibuni.

Ujerumani, Austria, Poland, Uholanzi na Ugiriki ni miongoni mwa mataifa ya kwanza ya Ulaya kuwasha tena mitambo ya kuzalisha nishati kwa kutumia makaa ya mawe au kuchukua hatua za kuunga mkono nishati inayotokana na makaa ya mawe, zikisisitiza umuhimu wa usalama wa usambazaji wa nishati katika majira ya baridi yanayokuja.

Hii inaashilia "kurudi nyuma" kwa juhudi za Ulaya katika miaka ya hivi karibuni za kuhimiza vyanzo vipya vya nishati, kuzuia uzalishaji wa nishati kwa kutumia makaa ya mawe ili kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na kupunguza uwiano wa nishati inayotokana na makaa ya mawe kwenye mchanganyiko wa nishati.

Hali isiyotarajiwa

Kamisheni ya Ulaya ilibainisha Jumatatu wiki hii kuwa "baadhi ya uwezo wa kuzalisha wa makaa ya mawe uliopo unaweza kutumika kwa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa awali" kwa sababu ya mazingira mapya ya nishati barani Ulaya.

"Tunajua kuwa mchanganyiko wa nishati na mipango ya nchi wanachama itabadilika kidogo kwa sababu tuko katika hali isiyotarajiwa," msemaji wa kamisheni hiyo Tim McPhie amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

Kampuni ya nishati ya Russia ya Gazprom hivi karibuni imepunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wa gesi kupitia bomba la Nord Stream 1 linalotoka Russia hadi Ujerumani.

Tayari nchi kadhaa za Ulaya zinazotegemea nishati kutoka Russia zimeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kupunguza matumizi ya gesi, kuanza kuwasha mitambo ya makaa ya mawe na kuchukua hatua za dharura kabla ya majira ya baridi kuanza.

"Kwa hakika, kwa miaka miwili ijayo, itakuwa na maana ya kuongeza uzalishaji wa nishati kwa kutumia makaa ya mawe ….ili kupuguza utegemezi wa gesi kwa muda mfupi," Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis alisema Mwezi Aprili.

Hatua za muda?

Mgogoro kati ya Russia na Ukraine umelazimisha nchi nyingi za Ulaya kufikiria upya usambazaji wao wa nishati. Zinasisitiza kwamba "kurudi nyuma” katika sera zao za nishati ni hatua ya muda mfupi na itasaidia kuepuka uhaba wa gesi katika majira yajayo ya baridi.

Serikali ya Ujerumani imesema kuwa mitambo ya kuzalisha nishati kwa kutumia gesi ilibadilishwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya makaa ya mawe ili kupunguza matumizi ya gesi, huku ikisisitiza kuwa “Kurudi Nyuma” ghafla kwa sera yake ya nishati haimaanishi kujiondoa kwenye mpango wa kuondokana na makaa ya mawe.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha