China yaitaka Marekani kusitisha mawasiliano rasmi na Taiwan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 29, 2022

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian jana Jumanne aliitaka Marekani kufuata kikamilifu kanuni ya kuwepo kwa China moja na nyaraka tatu za pamoja kati ya China na Marekani, na kusitisha aina yoyote ya mawasiliano rasmi na Taiwan.

Zhao ameyasema hayo katika mkutano na wanahabari akijibu swali kuhusu kile kiitwacho Pendekezo la Marekani na Taiwan kuhusu Biashara ya Karne ya 21.

"China inapinga kithabiti aina zote za mawasiliano rasmi kati ya eneo la Taiwan na nchi zilizo na uhusiano wa kidiplomasia na China, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo au kusaini makubaliano yanayohusiana na mamlaka ya nchi, ambayo kimuundo ni ya kiserikali. Msimamo huu ni wa siku zote na wazi," Zhao ameeleza.

Zhao ameongeza kuwa, kuna China moja tu duniani, na Taiwan ni sehemu isiyoweza kutengwa ya eneo la China. Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ndiyo serikali pekee ya halali inayowakilisha China nzima.

Msemaji huyo amesema kuwa Marekani lazima ifuate kanuni ya kuwepo kwa China moja na masharti ya nyaraka tatu za pamoja kati ya China na Marekani, kusitisha aina zote za mawasiliano rasmi na Taiwan, kusitisha mazungumzo ya makubaliano yenye athari kwenye mamlaka ya nchi na ambayo kimuundo ni ya kiserikali, na kujiepusha kutoa ishara zozote mbaya kwa nguvu ya kutaka Taiwan ijitenge na China.

"Tungependa pia kuwafahamisha viongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Taiwan kwamba wanahitaji kukata tamaa mara moja juu ya wazo kwamba wanaweza kujitenga kwa msaada wa Marekani, kwa sababu jinsi wanavyotamani zaidi, ndivyo kushindwa kwao kutakuwa na uchungu zaidi, " Zhao ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha