China kukabidhi jengo jipya la Bunge kwa Zimbabwe

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 30, 2022

Picha iliyopigwa Juni 29, 2022 ikionyesha Baraza la Seneti katika jengo jipya la Bunge la Zimbabwe lililopo eneo la Mlima Hampden Hill, Zimbabwe. Jengo jipya la Bunge la Zimbabwe, lililojengwa na kufadhiliwa kikamilifu na China kama zawadi kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika, sasa limekamilika na liko tayari kutumika. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)

HARARE - Jengo jipya la Bunge la Zimbabwe, lililojengwa na kufadhiliwa kikamilifu na China kama zawadi kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika, sasa limekamilika na liko tayari kutumika.

Ilichukua miezi 42 kukamilisha ujenzi wa mradi huo, badala ya muda uliopangwa awali wa miezi 32 kutokana na kukatizwa na UVIKO-19. Ujenzi ulianza Novemba 2018.

Likiwa kwenye eneo la Mlima wa kihistoria wa Hampden Hill, umbali wa kama kilomita 18 Kaskazini-Magharibi mwa Harare, Mji Mkuu wa Zimbabwe, jengo hilo lenye ghorofa sita ni sehemu ya usanifu mzuri ambao umeunganisha umaalumu wa nakshi za Zimbabwe na China.

Kampuni ya Ujenzi ya Shanghai (SCG), ambayo ni mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo, Jumatano wiki hii iliandaa kuwaongoza waandishi wa habari kutembelea katika jengo hilo kabla ya makabidhiano yake rasmi kwa Serikali ya Zimbabwe katika siku za usoni.

Meneja wa mradi kutoka SCG Cai Libo amesema kukamilika kwa mradi huo ni hatua kubwa kwa urafiki wa China na Zimbabwe ambao unaendelea kuchanua.

"Hakuna shaka kwamba jengo jipya la bunge litakuwa jengo la kihistoria nchini Zimbabwe na hata katika eneo lote la Kusini mwa Afrika," Cai amesema.

Ameeleza kuwa, jengo hilo jipya la bunge ni moja ya miradi muhimu katika ushirikiano kati ya China na Afrika, wenye lengo la kuimarisha urafiki na mshikamano kati ya watu wa Zimbabwe na China huku ukiboresha miundombinu bungeni kwa ajili ya huduma bora kwa watu wa Zimbabwe.

"Mradi huu unaunga mkono demokrasia nchini Zimbabwe kwa kiasi kikubwa huku ukipandisha hadhi ya nchi," Cai amesema.

Kukamilika kwa jengo hilo jipya la bunge, ambalo limetumia kwa kiasi kikubwa muundo wa magofu ya kihistoria ya Zimbabwe Kuu, pia kunaashiria kuanza kwa mji mkuu mpya wa nchi hiyo wakati huu ambapo Serikali ya Zimbabwe inapanga kuweka miundombinu jirani na eneo hilo kama vile maeneo ya makazi, vituo vya ununuzi na barabara za kufikika ili kujenga mji mpya unaojitegemea kwa lengo la kupunguza msongamano wa mji mkuu Harare.

Jengo hilo la kifahari lenye uwezo wa kuchukua watu 400 wakiwa wamekaa lina nafasi ya sakafu yenye mita za mraba 33,000, na sehemu kuu mbili - jengo la ofisi lenye ghorofa sita na jengo la bunge lenye ghorofa nne. Sehemu za majengo ya ofisi na bunge zimeunganishwa kwa madaraja matatu kwenye kila ghorofa.

Mtu akitembea na kupita jengo jipya la Bunge la Zimbabwe kwenye eneo la Mlima Hampden Hill, Zimbabwe, Juni 29, 2022. (Picha na Shaun Jusa/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha