Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU atoa wito wa juhudi za pamoja dhidi ya changamoto nyingi zinazoikabili Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 30, 2022

ADDIS ABABA - Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat ametoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana ili kutatua changamoto nyingi zinazoathiri Bara hilo.

Faki amesisitiza kwamba janga la UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama na ugaidi, pamoja na msukosuko uliopo sasa wa chakula unaohusishwa na mgogoro unaoendelea kati ya Russia na Ukraine ni miongoni mwa changamoto za pamoja zinazoathiri Bara la Afrika kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya AU iliyotolewa Jumanne jioni Faki amesema hayo katika kikao cha hivi punde zaidi cha Bunge la Afrika, ambapo amesisitiza haja ya kutumia umoja wa bara hilo kukabiliana na changamoto za pamoja zinazoathiri bara hilo.

"Katika hatua hii ya mabadiliko kwenye historia ya bara letu, ni muhimu zaidi kushikamana na mambo muhimu ... kujiweka karibu na muunganisho wetu kwa kupunguza tofauti zetu, kujiweka nyuma ya maadili yetu ya mshikamano, kunufaishana na maelewano ili kujitayarisha vizuri zaidi kukabiliana na changamoto kubwa zinazokabili bara letu," taarifa ya AU imemnukuu Faki akisema.

Aidha amesisitiza kuwa, hali isiyokuwa ya kifani katika bara hilo inayohusiana na changamoto za kisiasa na kidemokrasia, ambayo imesababisha nchi nne wanachama wa AU kusimamishwa uanachama wa umoja huo, pia inahitaji juhudi za pamoja.

"Changamoto hizi nyingi ni changamoto kubwa kwa dhamiri za wawakilishi wa watu wa Afrika, ambao ni nyinyi," Faki ameliambia Bunge la Afrika.

Bunge la Afrika (PAP) lilianzishwa ili kuhakikisha ushiriki kamili wa watu wa Afrika katika maendeleo ya kiuchumi na uunganishaji wa bara hilo.

Hata hivyo, Faki amesisitiza kwamba "Bunge la Afrika, licha ya matumaini makubwa ambayo limetoa, bado limekwama katika kutafuta msingi wake wa kweli na utendaji kazi mzuri."

"Ikikabiliwa na changamoto zinazohitaji juhudi za utatuzi na hitaji la uhamasishaji wa jumla, AU haiwezi kumudu anasa ya mgogoro ambao unaendelea ndani ya mojawapo ya vyombo vyake muhimu," Mahamat amesisitiza, akilenga Bunge la Afrika.

PAP imekusudiwa kuwa jukwaa la watu kutoka mataifa yote ya Afrika kushirikishwa katika mijadala na kufanya maamuzi kuhusu matatizo na changamoto zinazokabili bara hili. Makao makuu ya bunge hilo yako Midrand, Afrika Kusini.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha