Kiongozi wa Baraza la Mpito la Sudan asema jeshi linatarajia kukabidhi madaraka kwa serikali iliyochaguliwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Juni 30, 2022

KHARTOUM - Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mpito la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan Jumatano wiki hii amesema kwamba Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan vinatarajia serikali iliyochaguliwa kuchukua madaraka ya kuendesha nchi.

"Njia pekee ni ama kwa maafikiano ya kina ya kitaifa au uchaguzi, lakini si kwa wito wa maandamano na hujuma," Al-Burhan amesema wakati akikagua vitengo maalum vya kijeshi katika mji mkuu Khartoum, kwa mujibu wa taarifa ya baraza hilo.

Kiongozi huyo ametoa wito wa kutumia haki ya kujieleza kupitia maandamano ya amani ambayo yanalinda mali za umma na za kibinafsi na hayadhuru maslahi ya raia wengine.

Khartoum na miji mingine ya Sudan inatarajiwa kushuhudia maandamano makubwa ya kudai utawala wa kiraia leo Alhamisi.

Utaratibu wa pande tatu wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mamlaka ya Kiserikali inayohusu Maendeleo (IGAD) umepewa jukumu la kuwezesha mazungumzo ya ndani ya Sudan ili kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Sudan imekuwa ikikumbwa na mgogoro wa kisiasa tangu Al-Burhan, Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan, kutangaza hali ya hatari Oktoba 25, 2021 na kulivunja Baraza Kuu na serikali ya kiraia.

Nchi hiyo ya Afrika tangu wakati huo imekuwa ikishuhudia maandamano ya kudai kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha