Raisi na Putin waahidi kupanua ushirikiano kati ya Iran na Russia, kuhakikisha usalama wa kikanda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 20, 2022
Raisi na Putin waahidi kupanua ushirikiano kati ya Iran na Russia, kuhakikisha usalama wa kikanda
Rais wa Irani Ebrahim Raisi (Kulia) akisalimiana na Rais wa Russia Vladimir Putin aliyezuru Tehran, Iran, Tarehe 19 Julai 2022. (Tovuti ya Rais wa Irani/Kutumwa kupitia Xinhua)

TEHRAN - Rais wa Iran Ebrahim Raisi na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wamefanya mazungumzo mjini Tehran Jumanne wiki hii, ambapo wamekubaliana kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili na kupanua ushirikiano ili kuhakikisha usalama katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Rais wa Iran, mkutano huo umefanyika kufuatia ziara ya Putin mjini Tehran siku ya Jumanne mchana kwa ajili ya kushiriki kwenye mkutano wa pande tatu na mwenyeji wake Raisi na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuhusu suala la Syria.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, viongozi hao waliangazia maendeleo ya hivi karibuni katika uhusiano wa nchi hizo mbili, ambayo yameboreka kwa kiasi kikubwa baada ya rais Raisi kuingia madarakani, huku wakielezea kuridhishwa na kuongezeka kwa uhusiano, haswa katika sekta za uchumi, usalama, miundombinu, nishati, biashara na viwanda.

Marais hao wawili pia wameonyesha azma ya kuendeleza njia ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Wakipongeza mafanikio ya pamoja katika mapambano dhidi ya ugaidi, Raisi na Putin wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kikanda na ya nje ya kikanda, huku wakiweka bayana kwamba wameazimia kusaidia kuhakikisha usalama katika "nchi huru" za eneo hilo.

Akielezea nia ya nchi hizo mbili ya kupanua uhusiano kati yao kuwa "ya ajabu," Raisi amesema kuwa, baada ya mikutano yake na Putin huko Moscow mwishoni mwa Januari na Ashgabat mwishoni mwa Juni, ushirikiano kati ya Iran na Russia umeendelea kuakisi mwelekeo unaokua ambao unahitaji kuimarishwa zaidi.

Kuhusu "mafanikio" ya ushirikiano wa pande mbili katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria, rais huyo wa Iran amesema ushirikiano huo "unaweka msingi wa kuboresha usalama na utulivu wa kikanda."

Ameongeza kuwa, Iran na Russia zimethibitisha hali ya kuaminiana na nia zao madhubuti katika kupambana dhidi ya ugaidi kupitia ushirikiano.

Kwa upande wake Putin amesema ushirikiano kati ya Russia na Iran umeongezeka katika sekta tofauti hususan katika masuala ya usalama wa kimataifa na kuongeza kuwa, pande zote mbili zina sehemu kubwa sana kwenye juhudi za kutatua mgogoro wa Syria.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha