Sunak, Truss waibuka washindi kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya Waziri Mkuu wa Uingereza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 21, 2022
Sunak, Truss waibuka washindi kwenye kinyang'anyiro cha nafasi ya Waziri Mkuu wa Uingereza
Waziri Mkuu wa Uingereza anayemaliza muda wake Boris Johnson (wa tatu kutoka kushoto, mbele) akiongoza mkutano wake wa mwisho wa baraza la mawaziri kwenye chumba cha baraza la mawaziri Mtaa No. 10 wa Downing huko London, Uingereza, Julai 19, 2022. (Andrew Parsons/Mtaa No. 10 wa Downing /Kutumwa kupitia Xinhua)

LONDON - Aliyekuwa Waziri wa Fedha Rishi Sunak na Waziri wa Mambo ya Nje wa wa Uingereza Liz Truss wameibuka wagombea wawili wa mwisho katika kinyang'anyiro cha uongozi wa Chama cha Conservative siku ya Jumatano.

Waziri wa Biashara ya Kimataifa Penny Mordaunt aliondolewa katika duru ya mwisho ya kura za wabunge wa Conservative. Sunak amepata kura 137, Truss amepata 113.

Kinyang'anyiro cha kuchukua nafasi ya Boris Johnson ya waziri mkuu sasa kitaenda mbele ya wanachama hai wa Chama cha Conservative wapatao 200,000, ambao watamchagua mshindi baadaye wakati wa msimu huu wa joto kupitia kura ya kutumwa kwa posta. Mshindi, atakayetangazwa Septemba 5, atakuwa mrithi wa Johnson moja kwa moja.

Ingawa Sunak ameshinda kila awamu tano za upigaji kura wa wabunge, kura ya maoni iliyoendeshwa na YouGov na kuchapishwa Jumanne wiki hii ilionyesha kuwa hakuwa maarufu sana miongoni mwa wanachama wa mashinani wa chama hicho. Anatabiriwa kushindwa na Truss, kipenzi cha mrengo wa kulia wa chama, katika uchaguzi huo wenye ushindani mkali.

Wagombea wote wawili wametoa ahadi za kupunguzwa kwa ushuru huku msukosuko wa gharama za maisha ukiendelea kuuma. Hata hivyo, Sunak alipuuzilia mbali "hadithi" za ahadi za wapinzani wake za kupunguzwa kwa kodi mara moja, akisema kuwa mfumuko wa bei lazima udhibitiwe kwanza. Takwimu rasmi zilionyesha Jumatano kwamba, mfumuko wa bei nchini Uingereza ulipanda kwa asilimia 9.4 Mwezi Juni, na kufikia kiwango cha juu katika miaka 40 iliyopita.

Truss, kwa upande mwingine, aliahidi kuanza kupunguza ushuru siku ya kwanza tu akianza kazi.

Kinyang'anyiro cha uongozi wa Chama cha Conservative kimechochewa baada ya Johnson kulazimishwa kuachia ngazi Julai 7 kutokana na kujiuzulu kwa mkupuo maafisa wa serikali, ambao walipinga uongozi wake uliokumbwa na kashfa. Johnson anaendelea kuhudumu kama waziri mkuu wa muda hadi kiongozi mpya atakapatikana.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha