China kuchukua hatua kali ikiwa Spika wa Bunge la Marekani Pelosi atasisitiza kuzuru Taiwan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2022

(Picha inatoka tovuti ya Shirika la Habari la China Xinhua.)

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin Alhamisi wiki hii amesema kwamba China itachukua hatua madhubuti kujibu kwa uthabiti ziara iliyopangwa ya Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi kwenda eneo la Taiwan la China na itachukua hatua za kukabiliana iwapo upande wa Marekani utasisitiza kufanya ziara hiyo.

“Upande wa China umerudia kueleza msimamo wake mkali wa kupinga kithabiti ziara ya Pelosi kisiwani Taiwan,” Wang amesema kwenye mkutano wa kila siku na waandishi wa habari, na kuongeza kuwa Bunge la Marekani ni sehemu ya Serikali ya Marekani, na linapaswa kuzingatia kikamilifu ahadi ya Marekani juu ya suala la Taiwan.

"Iwapo Spika Pelosi atazuru Taiwan, itakiuka sana kanuni ya kuwepo kwa China moja na masharti katika nyaraka tatu za makubaliano ya pamoja kati ya China na Marekani na kuathiri mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya China," Wang amesema.

Wang amesema itakuwa na athari mbaya kwa msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Marekani, na kutuma ishara mbaya sana kwa vikundi vya kutaka Taiwan ijitenge na China.

"Iwapo upande wa Marekani utasisitiza kufanya ziara hiyo, China itachukua hatua madhubuti kujibu kwa uthabiti na kuchukua hatua za kukabiliana. Tunamaanisha kile tunachosema," Wang amesema.

Mwezi Aprili mwaka huu spika huyo wa Bunge la Marekani alipanga kuzuru eneo la Taiwan, kitendo ambacho kilipingwa na kulaaniwa vikali na Balozi wa China nchini Marekani Qin Gang. Katika taarifa yake Qing aliitaka Marekani kufuta mara moja ziara hiyo.

Hata hivyo, ziara hiyo ya Pelosi iliahirishwa mwezi huo wa Aprili baada ya kiongozi huyo wa Bunge la Marekani kukutwa na maambukizi ya virusi vya Korona siku chache kabla ya siku ya ziara hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha