Waziri Mkuu wa Italia Draghi ajiuzulu, uchaguzi mpya kufanyika Septemba 25

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2022
Waziri Mkuu wa Italia Draghi ajiuzulu, uchaguzi mpya kufanyika Septemba 25
Waziri Mkuu wa Italia Mario Draghi akiwapungia mkono wabunge mwishoni mwa hotuba yake kwenye ukumbi wa bunge la baraza la chini mjini Rome, Italia, Julai 21, 2022. (Picha na Alberto Lingria/Xinhua)

ROME – Ikulu ya Italia imetangaza Alhamisi wiki hii kuwa, nchi hiyo itafanya uchaguzi Septemba 25 kabla ya wakati uliopangwa, baada ya Waziri Mkuu Mario Draghi kujiuzulu na kuvunjwa kwa bunge.

Kujiuzulu kwa Draghi kumefanya serikali yake ya umoja wa kitaifa iliyoundwa Mwezi Februari 2021 kwa kuungwa mkono na muungano mpana kufikia mwisho. Uamuzi wake wa kujiuzulu umekuja baada ya washirika watatu wakuu katika muungano huo kutoshiriki katika upigaji kura ya kutokuwa na imani kwenye Bunge la Seneti siku ya Jumatano, hivyo basi kuondoa uungaji mkono wao kwa baraza la mawaziri.

Chaguo la mwisho

Rais wa Italia Sergio Mattarella alitangaza kuvunjwa mapema kwa mabaraza mawili ya bunge Alhamisi mchana, baada ya Draghi kukubali kujiuzulu kupitia hotuba fupi kwa taifa.

Mattarella amesisitiza kuvunja mabunge mapema kabla ya wakati "daima lilikuwa chaguo la mwisho kufanya," lakini alielezea hatua hii kuwa isiyoweza kuepukika kwani kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu ya Jumatano kwenye Bunge la Seneti ilithibitisha "kukosekana kwa mtazamo wowote wa kuunda muungano wa vyama vyenye wabunge wengi."

Hata hivyo alionya vyama vya kisiasa kwamba nchi hiyo inakabiliwa na changamoto muhimu ambazo haziwezi kusitishwa.

Uchaguzi wa aina yake majira ya Autumn

Raia wa Italia sasa watapiga kura katika majira ya Autumn. Kwenye hotuba yake Alhamisi, Mattarella alisema uchaguzi wa mapema utakuja wakati nyeti sana kwa Italia na Ulaya.

Mgogoro ambao umesababisha kuvunjika kwa baraza la mawaziri la Draghi ulichochewa wiki iliyopita na Five Star Movement (M5S) kuhusu muswada wa serikali wa kuleta unafuu wa kiuchumi wenye thamani ya takriban euro bilioni 26 (karibu dola bilioni 26.5 za Kimarekani) kusaidia makampuni na familia kukabiliana na bili za nishati na gharama nyinginezo za maisha zinazoongezeka.

Chama kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Giuseppe Conte, kilisema bajeti hiyo haitoshi na kiligomea kupiga kura.

Kwenye mwenendo wa kura ya kutokuwa na imani katika Bunge la Seneti siku ya Jumatano, chama cha Ligi cha mrengo wa kulia na chama cha mrengo wa kulia-kati cha Forza Italia vilijiunga na M5S katika kugomea upigaji kura hivyo kuifanya serikali ya Draghi ikose uungwaji mkono.

Baraza la mawaziri la Draghi litasalia madarakani kama msimamizi wa mambo ya serikali hadi baraza lingine litakapoundwa baada ya uchaguzi. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha