Bomba la Nord Stream 1 kusafirisha tena gesi kwenda Ujerumani baada ya matengenezo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 22, 2022
Bomba la Nord Stream 1 kusafirisha tena gesi kwenda Ujerumani baada ya matengenezo
Rais wa Kamati ya Ulaya Ursula von der Leyen akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji, Julai 20, 2022. (Xinhua/Zheng Huansong)

BERLIN - Baada ya bomba la Nord Stream 1 kuwa kwenye ukarabati kwa siku kumi, usafirishaji wa gesi kutoka Russia hadi Ujerumani umeanza tena Alhamisi asubuhi.

"Nord Stream AG imekamilisha kwa ufanisi kazi zote za ukarabati zilizopangwa kwenye mabomba yake mawili ya gesi ndani ya muda uliopangwa," mwendeshaji wa bomba hilo alisema kwenye taarifa.

Ingawa kumiminika kwa gesi sasa kumefikia kiwango cha awali cha kabla ya ukarabati, ambacho kinalingana na asilimia 40 ya matumizi ya jumla ya uwezo wa bomba hilo, kiwango kinachokosekana na ukosefu wa utulivu wa kisiasa hautoi "sababu ya kusema kila kitu kiko tayari," amesema Klaus Mueller, rais wa Federal Network Agency (BNetzA).

"Tunahitaji (kuvuta) pumzi ndefu, majira ya baridi bado hayajafika," Waziri wa Masuala ya Uchumi na Hatua za Tabianchi wa Ujerumani, Robert Habeck amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Habeck ametangaza hatua zaidi za kuhifadhi nishati, ikiwa ni pamoja na mahitaji makali zaidi ya kujaza vituo vya kuhifadhi gesi, ambayo katika siku zijazo lazima ifikie asilimia 95 ya uwezo ifikapo Novemba 1, kutoka asilimia 90 ya hapo awali.

Kwa mujibu wa BNetzA, hivi sasa, vituo vya kuhifadhi gesi nchini Ujerumani vimejazwa kwa asilimia 65.1. Hata hivyo, ikiwa usambazaji wa gesi ya Russia utaendelea katika kiwango hiki cha chini, "haitawezekana kufikia kiwango cha hifadhi cha asilimia 90 ifikapo Novemba bila hatua za ziada."

Idara ya Takwimu ya Ujerumani ilisema Alhamisi kwamba, gesi asilia ni "chanzo kikuu cha nishati" kwa viwanda na kaya nchini Ujerumani. Mwaka 2020, asilimia 31 ya sekta ya viwanda ya Ujerumani ilitumia gesi asilia.

Bei ya gesi barani Ulaya imeshuka baada ya kuanza tena kwa usambazaji wa gesi ya Russia kupitia bomba la Nord Stream 1.

"(Kuanza tena kwa) usambazaji wa gesi kutoka Russia kupitia bomba muhimu la kimkakati la Nord Stream 1 ndiyo sababu (hii)," Christoph Schmitz wa taasisi ya r2b ya ushauri wa nishati ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua siku ya Alhamisi.

Baada ya uvumi fulani kwamba Russia inaweza kutumia kazi ya ukarabati kama kisingizio cha kusimamisha usafirishaji kwa muda mrefu kuliko ilivyokubaliwa kimkataba, "matarajio ya uwasilishaji upya yaliongezeka katika siku za hivi majuzi," amesema Schmitz.

Kamati ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza siku ya Jumatano kwamba nchi wanachama zinapaswa kupunguza kwa hiari mahitaji yao ya gesi kwa asilimia 15 ili kupunguza hali ya uhaba wa usambazaji. Hata hivyo, kuna chaguo la kulazimisha kupunguza mahitaji kwa kutangaza "Tahadhari ya Umoja." 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha