China yasema jeshi lake halitakaa kimya kama Spika wa Bunge la Marekani Pelosi atazuru Taiwan

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 27, 2022

BEIJING – Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China Tan Kefei Jumanne wiki hii alionya kuwa Jeshi la China halitakaa kimya kama Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi atazuru eneo la Taiwan la China.

Tan alitoa kauli hiyo alipojibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu suala hilo.

China inaitaka Marekani kuheshimu ahadi yake kwamba haitaunga mkono Taiwan ijitenge," Tan alisema, na kuongeza kuwa ikiwa upande wa Marekani utasisitiza kufanya ziara hiyo, Jeshi la China litachukua hatua kali kuzuia uingiliaji wowote wa nje au mpango wowote wa makundi yanayotaka Taiwan ijitenge, na italinda kithabiti mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya China.

Tan alisema upande wa China umerudia kueleza wazi kwa Marekani upinzani wake thabiti kwa ziara inayowezekana ya Pelosi kwenye eneo la Taiwan.

"Iwapo Spika Pelosi atazuru Taiwan, itakiuka sana kanuni ya kuwepo kwa China moja na masharti katika nyaraka tatu za pamoja kati ya China na Marekani, kuathiri vibaya mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi ya China, na kuharibu kwa kiasi kikubwa msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Marekani," Tan alisema.

Msemaji huyo alieleza kuwa, kama ziara hiyo itafanyika hakika itasababisha uharibifu mkubwa sana kwenye uhusiano kati ya nchi hizo mbili na wa majeshi ya nchi hizo, na kusababisha hali ya wasiwasi inayozidi kuwa mbaya katika Mlango-Bahari wa Taiwan.

Mwezi Aprili mwaka huu spika huyo wa Bunge la Marekani alipanga kuzuru eneo la Taiwan, kitendo ambacho kilipingwa na kulaaniwa vikali na Balozi wa China nchini Marekani Qin Gang. Katika taarifa yake Qing aliitaka Marekani kufuta mara moja ziara hiyo.

Hata hivyo, ziara hiyo ya Pelosi iliahirishwa mwezi huo wa Aprili baada ya kiongozi huyo wa Bunge la Marekani kukutwa na maambukizi ya virusi vya Korona siku chache kabla ya siku ya ziara hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha