Marais wa Cameroon na Ufaransa wajadili usalama wa kikanda, uhusiano wa kiuchumi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 27, 2022
Marais wa Cameroon na Ufaransa wajadili usalama wa kikanda, uhusiano wa kiuchumi
Rais wa Cameroon Paul Biya (kulia, mbele) akimkaribisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kati, mbele) mjini Yaounde, Cameroon, Julai 26, 2022. Rais wa Cameroon Paul Biya Jumanne wiki hii alikutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayezuru Yaounde ili kujadili usalama wa kikanda na uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. (Xinhua/Kepseu)

YAoundE - Rais wa Cameroon Paul Biya Jumanne wiki hii alikutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayezuru mjini Yaounde ili kujadili usalama wa kikanda na uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wao, Macron alisema Cameroon ni "mbia wa kimkakati" katika eneo la Afrika ya Kati ambalo "atalipa kipaumbele zaidi katika muhula wa pili."

Macron amesema nchi yake itaendelea kuunga mkono hitaji la Afrika kuhusu usalama na utulivu. "Hatutaacha usalama wa Bara la Afrika, sasa tuna mfumo wa ushirikiano wa kijeshi na nchi nyingi za Afrika, na hii ina maana kwamba tunatoa vifaa, tunatoa mafunzo, tuna ushirikiano na tunataka kusonga mbele katika mwelekeo huo,"

"Ninahisi kuridhika kwa sababu tunahisi kuungwa mkono. Ufaransa inatuunga mkono kwa maana ya usalama, hasa kuhusu vita dhidi ya ugaidi," Biya amesema.

Marais hao pia wamejadili uhaba wa chakula barani Afrika. Macron amesema Ufaransa itaimarisha uwekezaji na ushirikiano wa kilimo ikiwa ni sehemu ya hatua za kutatua msukosuko wa chakula.

Cameroon imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa waasi wenye silaha wanaotaka kujitenga katika maeneo yake ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi yanayozungumza Lugha ya Kiingereza tangu Mwaka 2017.

"Bado ninashawishika kuwa uimarishaji wa kikanda utaendelea kuwa jibu la mgogoro unaoathiri Cameroon katika maeneo ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi na kwamba ni kupitia mchakato huu wa kisiasa wa mazungumzo na mageuzi ndipo suluhu ya kudumu inaweza kupatikana," Macron amesema.

Rais huyo wa Ufaransa amewasili Cameroon Jumatatu usiku kuanza ziara yake ya kwanza rasmi barani Afrika baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili na wa mwisho Mwezi Aprili. Pia atazuru Benin na Guinea-Bissau. 

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha