Macron asisitiza uungaji mkono wa Ufaransa katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Benin

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 28, 2022

Rais wa Benin Patrice Talon (Kulia) na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari huko Cotonou, Benin, Julai 27, 2022. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)

COTONOU - Rais wa Benin Patrice Talon na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron Jumatano wiki hii wameahidi kupambana dhidi ya ugaidi nchini Benin na ukanda mdogo wa Afrika Magharibi.

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Cotonou, Rais Talon amesema kuwa changamoto inayoikabili Benin hivi sasa ni mapambano dhidi ya ugaidi hasa katika eneo la Kaskazini mwa nchi yake.

"Rais wa Ufaransa Macron na mimi tumekubaliana kwamba Ufaransa itatuunga mkono zaidi katika juhudi zetu za kupambana dhidi ya ugaidi kwa sababu kwa sasa ugaidi ni mojawapo ya changamoto zetu kuu," amesema.

Kwa upande wake, Macron amesisitiza tena kwamba "Ufaransa daima itakuwa upande wa Serikali ya Benin ili kukabiliana na vitisho hivi. Tutasikiliza maombi yenu."

“Kwa upande wa usalama, kwa mujibu wa upangaji upya ambao tumeupitisha katika ukanda mdogo wote, tutatimiza maombi yenu kwa upande wa mafunzo na vifaa,” amesema.

Macron aliwasili Cameroon Jumatatu usiku kuanza ziara yake rasmi ya kwanza barani Afrika baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili na wa mwisho Mwezi Aprili. Baada ya ziara yake nchini Benin, pia atazuru Guinea-Bissau leo Alhamisi.

Rais wa Benin Patrice Talon (kulia, mbele) akimkaribisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto, mbele) mjini Cotonou, Benin, Tarehe 27 Julai 2022. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha