Kongamano la Vyombo vya Habari kuhusu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lafanyika kwa mafanikio Shaanxi, China

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 10, 2022
Kongamano la Vyombo vya Habari kuhusu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lafanyika kwa mafanikio Shaanxi, China
Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya CPC Huang Kunming akitoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Kongamano la Sita la Vyombo vya Habari kuhusu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” huko Shaanxi China Agosti 9, 2022 (Picha: People’s Daily Online)

Kongamano la Sita la Vyombo vya Habari kuhusu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limefanyika kwa mafanikio makubwa katika Mji wa Xi’an, Mkoa wa Shaanxi nchini China na kuhudhuriwa kwa njia ya intaneti na nje ya intaneti na wageni mbalimbali mashuhuri kutoka ndani na nje ya China.

Kongamano hilo limefanyika baada ya ziara za kikazi za waandishi wa habari kutoka ndani na nje ya China Mkoani Shaanxi nchini China ambapo walifanya ukaguzi, mahojiano, utafiti na majadiliano kwenye miradi na uwekezaji mbalimbali wa kimkakati kwenye maeneo ya kiuchumi yaliyounganishwa na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”.

Akitoa hotuba kuu ya ufunguzi wa kongamano hilo kwa njia ya video, Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Huang Kunming amesisitiza kwamba ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umekuwa bidhaa ya umma na jukwaa la ushirikiano wa kimataifa.

"Katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, kasi ya uunganisho wa miundombinu na muundo wa miunganisho katika ardhi, bahari na angani imekuwa bora na bora. Pia makubaliano ya kisheria na viwango yamepata matokeo ya ajabu. China imesaini makubaliano zaidi ya 200 ya ushirikiano na nchi 149 na mashirika 32 ya kimataifa. Kwa mantiki hii, kiwango cha kufungua mlango na uwezeshaji wa biashara kinaendelea kuboreka na vyombo vya habari vina jukumu lisiloweza kubadilishwa kufikia malengo haya”, amesema Huang.

Tuo Zhen, Mkuu wa People's Daily, amesisitiza kuwa Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” limetoka kuwa dhana na maono hadi hatua katika uhalisia.

"Vyombo vya habari vya nchi mbalimbali vinaweza kutumia vyema jukwaa hili, kuwasilisha maoni ya umma na kuimarisha uelewa wa pamoja na kuaminiana."

Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Independent Media (pty) ya Afrika Kusini, Iqbal Surve amesema kuwa Dunia ya sasa inakumbwa na migogoro mingi ambayo inatishia uchumi wa Dunia kuingia kwenye mdororo.

Katika hili amesema, kongamano la vyombo vya habari la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lina jukumu la kuimarisha kwa kina ushirikiano na kuhakikisha kwamba habari muhimu zinawafikia watu kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Tunahitaji habari za kina, sahihi na za ukweli ambazo zitaimarisha uhusiano na maingiliano kati ya watu” amesema.

Naye Teo Lay Lim, Mkurugenzi Mtendaji wa SPH Media Trust ya Singapore amesema Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ni muhimu sana katika kukuza uchumi na biashara duniani. Amesema kuwa, chini ya “Ukanda Mmoja, Njia Moja” maeneo makuu manne yameshuhudia maendeleo makubwa ambayo ni pamoja na uunganisho wa miundombinu, uunganisho wa kifedha, watu wa upande wa tatu kupata manufaa na ushirikiano wa kitaalamu.

Teo ametoa mapendekezo manne katika ujenzi wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ambayo ni uwazi na ujumuishi, uendelevu, uzingatiaji wa mazingira na uchumi wa kijani, na uhusiano na maelewano mazuri.

Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ambalo kwa sasa linaleta mageuzi makubwa katika diplomasia na uhusiano wa kimataifa, lilitangazwa Mwaka 2013 na Rais wa China, Xi Jinping. Katika miaka michache tu tangu litangazwe, pendekezo hili limebadilika kutoka dhana hadi hatua, kutoka maono hadi ukweli, na kutoka mpango hadi mafanikio halisi ya Dunia.

Gazeti la People's Daily ndilo huandaa kongamano hilo na limefanyika huko nyuma katika miaka ya 2014, 2015, 2016, 2017 na 2018, ili kujenga mazungumzo na majadiliano ya hadhi ya juu.

Kongamano la mwaka huu ambalo limebeba kaulimbiu ya “Kujikita katika Maendeleo ya Dunia na Kuhimiza Muunganisho" limeandaliwa kwa pamoja na People’s Daily, Serikali ya Mkoa wa Shaanxi na Kamati ya Chama ya Mkoa wa Shaanxi.

Mbali na kongamano kuu, kumefanyika mijadala pacha kuhsusu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Katika mjadala wa kwanza, mada kuhusu Wajibu wa Vyombo vya Habari katika kuhimiza maendeleo ya Dunia iliwasilishwa na wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo China. Mjadala wa pili; ulihusisha mada kuhusu Maendeleo yanashikilia ufunguo wa maisha bora ya watu. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha