M23 bado yaendelea kushikilia maeneo iliyoyateka Kaskazini Mashariki mwa DRC licha ya amri ya kuwataka kujiondoa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 01, 2022
M23 bado yaendelea kushikilia maeneo iliyoyateka Kaskazini Mashariki mwa DRC licha ya amri ya kuwataka kujiondoa
Picha iliyopigwa Novemba 21, 2022 ikionyesha wanajeshi wakishiriki kwenye operesheni karibu na Kibumba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). (Xinhua/Alain Uaykani)

GOMA, DRC - Waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23) bado wamegoma kuondoka katika maeneo wanayokalia Kaskazini-Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), licha ya muda wa mwisho uliowekwa na Kinshasa wa kuwataka kujiondoa, mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la China, Xinhua ameshuhudia moja kwa moja.

Huku mapigano yakiendelea kushika kasi kati ya waasi na jeshi la serikali, DRC inategemea njia ya kidiplomasia kuleta amani, hasa awamu ya tatu ya mazungumzo yanayoendelea tangu Jumatatu mjini Nairobi, na kuleta makundi kadhaa yenye silaha kwenye meza ya mazungumzo isipokuwa M23.

M23 yapewa muda mwisho kujiondoa

Tangu Mei 2022, waasi wa M23 wameteka vijiji kadhaa katika jimbo la Kaskazini Mashariki mwa DRC la Kivu Kaskazini. Wiki iliyopita, M23 na Jeshi la DRC walipigana huko Kibumba, iliyoko umbali wa takriban kilomita 20 kutoka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini na mji mkubwa zaidi Mashariki mwa DRC.

Novemba 23, mkutano mdogo wa kilele uliofanyika huko Luanda, mji mkuu wa Angola, ambao Rais wa DRC Felix Tshisekedi pia alishiriki, uliweka ratiba iliyotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano na juu ya yote uamuzi wa kuwataka waasi wa M23 kujiondoa katika maeneo wanayoyakalia.

Hakuna dalili za M23 kujiondoa hata hivyo, amri ya mwisho wa M23 kujiondoa bado haijazaa matunda, amebainisha mwandishi wa Xinhua moja kwa moja kutoka eneo la mapigano la Kibumba.

“Wapo mbele yetu kwa sababu hawakutii amri ya kujiondoa, na tunatazamana nao usiku na mchana. Usitishaji wa mapigano bado si madhubuti kwa sasa, tunaendelea kushikilia maeneo yetu kutokana na amri kutoka ngazi za juu kutii maagizo ya mamlaka ya kikanda," Ndjike Kaiko, msemaji wa jeshi katika eneo hilo, ameliambia Xinhua.

Katika lango la kuingia Kibumba, baadhi ya wanajeshi wametumwa kwenye operesheni maalum ya kuzuia kusonga mbele kwa waasi huko Goma. Takriban wiki moja iliyopita, mapigano yalizuka tena kuhusu eneo hili wakati waasi walipojaribu kuingia Goma.

"Tuko tayari kwa tukio lolote kwenye mstari huu ambao unachukuliwa kuwa kufuli kuu kuelekea mji wa Goma. Waasi hawa hawasikii sauti ya kidiplomasia, wanataka kupigana tu, na kwa hilo, kama jeshi, tuko pale kulinda nchi yetu dhidi ya wavamizi," afisa mmoja aliyeko kwenye mipaka ya maeneo ya waasi alisema.

Mazungumzo bila M23

Tangu Jumatatu mjini Nairobi, mazungumzo kati ya makundi yenye silaha na Serikali ya DRC yameanza tena chini ya mwamko wa mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kukomesha mzunguko wa vurugu na kurejesha amani na usalama katika eneo hili la DRC.

Wawakilishi kadhaa wa wanamgambo wa eneo hilo wamefanya safari ili kushiriki katika mikutano hii, isipokuwa waasi wa M23 ambao hawakualikwa kwa ombi la Serikali ya DRC, ambayo hapo awali iliwataka wajiondoe kwanza katika maeneo yaliyokuwa chini ya uvamizi kama sharti la kushiriki mazungumzo.

Takriban watu 200,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha