Algeria na Jordan zatia saini mikataba 5 ya kuimarisha uhusiano

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 05, 2022
Algeria na Jordan zatia saini mikataba 5 ya kuimarisha uhusiano
Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune (Kulia) akikutana na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan anayezuru mjini Algiers, Algeria, Desemba 4, 2022. Algeria na Jordan zimetia saini mikataba mitano siku ya Jumapili katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune na Mfalme Abdullah II wa Jordan anayezuru katika mji mkuu wa Algiers. (Ikulu ya Algeria/Kutumwa Xinhua)

ALGIERS - Algeria na Jordan zimetia saini mikataba mitano siku ya Jumapili katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune na mgeni wake rasmi Mfalme Abdullah II wa Jordan katika mji mkuu wa Algiers.

Makubaliano hayo yamejumuisha mkataba wa maelewano (MoU) kuhusu mashauriano ya kisiasa baina ya nchi hizo mbili, makubaliano ya msamaha wa visa vya pande zote kwa raia wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na Maelewano kati ya taasisi za kidiplomasia za nchi hizo mbili.

Nchi hizo mbili pia zimekubaliana kuanzisha mpango wa ushirikiano wa pamoja kati ya mashirika rasmi ya habari ya Algeria na Jordan, na kutambua kwa pande zote vyeti vya kustahiki vinavyotolewa kwa mabaharia na programu za mafunzo ya baharini.

Mapema siku hiyo, mawaziri wa Algeria na Jordan walifanya mazungumzo na kujadili njia za kukuza uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya kibiashara.

Algiers na Amman zimeonyesha nia yao ya kukuza uhusiano wa nchi mbili. Jordan ni mshirika wa sita wa biashara wa Algeria katika eneo la Kiarabu, na mabadilishano ya kibishara yanayofikia jumla ya dola za Kimarekani milioni 219.24 Mwaka 2021, Shirika la Habari la Algeria, APS limeripoti.

Mfalme Abdullah II wa Jordan aliwasili Algiers Jumamosi jioni kwa ziara ya kiserikali kwa mwaliko wa Rais wa Algeria.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha