Ujenzi wa Makao Makuu ya Kudumu ya ECOWAS unaofadhiliwa na kujengwa na China waanza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 05, 2022
Ujenzi wa Makao Makuu ya Kudumu ya ECOWAS unaofadhiliwa na kujengwa na China waanza
Ujenzi wa Makao Makuu ya Kudumu ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) unaofadhiliwa na kujengwa na China umeanza Jumapili katika Mji Mkuu wa Nigeria, Abuja tarehe 4, Desemba. (Picha/Xinhua)

Ujenzi wa Makao Makuu ya Kudumu ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) unaofadhiliwa na kujengwa na China umeanza Jumapili katika Mji Mkuu wa Nigeria, Abuja, hivyo kuelekea kuzifanya shughuli za jumuiya hiyo kufanyika kwenye jengo moja kuliko ilivyo sasa ambapo zinafanyika kwa kuhamahama sehemu tatu tofauti katika Mji wa Abuja.

Walau viongozi watatu wa Afrika Magharibi akiwemo Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na marais wenzake wa Guinea Bissau na Sierra Leone vilevile na Rais wa Kamisheni ya ECOWAS Omar Alieu Touray na Balozi wa China nchini Nigeria Cui Jianchun wameshiriki kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi na kuanzisha rasmi ujenzi wa makao makuu hayo.

“Kufadhili na kujenga makao makuu mapya ya ECOWAS ni ushahidi wa wazi wa uungaji mkono wa China kwenye kazi za ECOWAS, vilevile urafiki wa jadi kati ya China na nchi za Afrika Magharibi,” Cui amesema.

Rais Buhari ameuelezea mradi huo kama “alama ya China kujitolea kwa ECOWAS”, akisema kwamba mradi huo utakapokamilika, utaziweka pamoja taasisi kuu tatu za jumuiya hiyo ikiwemo sekretarieti ya ECOWAS, Mahakama ya Haki ya ECOWAS na Bunge la ECOWAS.

Rais Buhari amesema mradi huo unaojengwa na Kampuni ya China, utakuwa “makao makuu na eneo la mikutano ya jumuiya” huku ukiwakilisha umoja na undugu wa nchi wanachama, vilevile, kuashiria kujitolea tena kwa maendeleo na ushirikiano wa kikanda.

Hafla hiyo ya kuweka jiwe la msingi inaashiria "siku muhimu sana katika historia ya ECOWAS," Touray amesema, huku pia akitoa shukrani kwa serikali ya China.

Amesema makao makuu hayo mapya yatawezesha Kamisheni ya ECOWAS kuhudumia wafanyakazi wake wote katika eneo moja, jambo ambalo litasababisha zaidi "ufanisi wa utendaji kazi, kupunguza gharama na kuongeza tija." 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha