Rais wa Msumbiji azindua mitambo ya uzalishji ya mradi wa uchimbaji mchanga mzito uliowekezwa na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 05, 2022

MAPUTO - Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi Ijumaa alizindua mitambo miwili ya mradi wa uzalishaji wa mchanga mzito uliowekezwa na Kampuni ya Madini ya China ya Ding Sheng katika Wilaya ya Chibuto ya Jimbo la Kusini mwa Msumbiji la Gaza.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa kampuni hiyo, Lin Wenwen, kwa kuanzishwa rasmi kwa mitambo hiyo miwili mipya ya uzalishaji ukiongeza mitambo ya zamani ya uzalishaji iliyokuwepo, Kampuni ya Madini ya Ding Sheng imefikia uwezo wa uzalishaji wa zaidi ya tani milioni 1.8 za madini ya titanium na zirconium kwa mwaka.

Katika hafla hiyo, Rais Nyusi aliona sampuli za mchanga wa madini zilizokuwa zikionyeshwa na kutembelea mitambo ya uzalishaji kwenye moja ya maeneo ya uchimbaji.

Katika hotuba yake iliyofuata, Rais Nyusi amepongeza ufanisi wa uendeshaji wa mradi huo na kusema hatua zilizochukuliwa na kampuni hiyo kulinda mazingira katika eneo la uchimbaji madini na kuwanufaisha watu wa eneo hilo ni za kupongezwa. Alikuwa akizungumzia nyumba za makazi mapya na kituo cha kuchakata maji ambacho kinaweza kutoa maji ya bomba kwa wakazi 200,000, miongoni mwa vituo vingine vilivyojengwa na kampuni hiyo.

“Tuna uhakika kutokana na ukubwa wa mradi huu, eneo la Chibuto litakuwa kitovu cha maendeleo chenye miundombinu itakayoendelezwa kwa shughuli nyingine za kiuchumi katika mnyororo wa uendeshaji na usafirishaji wa miradi ya mchanga mzito,” amesema Rais.

Amesema mradi huo umetoa nafasi za ajira 3,000 kwa wafanyakazi wa Msumbiji na wageni wakati wa mchakato wa ujenzi wake huku akitoa shukrani kwa China kwa kuleta uwekezaji nchini mwake.

Rais amesisitiza kuwa Msumbiji ina rasilimali nyingi za madini na kwamba pamoja na miradi mingine katika sekta ya uziduaji, mradi wa Chibuto utachangia katika hazina ya serikali na ukuaji wa pato la taifa.

“Tumekuwa tukishirikiana na Serikali ya China kuona kama tunaweza kuhamasisha wawekezaji zaidi katika eneo la Chibuto ambalo hapo baadaye litakuwa kituo bora cha viwanda,” amesema Nyusi.

Katika hotuba yake kwenye hafla hizo, Balozi wa China nchini Msumbiji Wang Hejun amesema mradi huo utahimiza zaidi matumizi bora ya rasilimali za Msumbiji, na kuisaidia Msumbiji kubadilisha rasilimali yake ya juu kuwa msukumo wa kweli wa ukuaji wa uchumi.

“Ninaamini kuwa chini ya uongozi wa wakuu wetu wa nchi na kwa juhudi za pamoja za serikali na watu wetu, ushirikiano wa kivitendo kati ya China na Msumbiji katika nyanja mbalimbali bila shaka utatoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hizo mbili na uboreshaji endelevu wa ustawi wa watu,” amesema balozi huyo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha