Viongozi wa kijeshi na wa kiraia wa Sudan watia saini makubaliano ya kumaliza msukosuko wa kisiasa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 06, 2022

KHARTOUM - Viongozi wa kijeshi na kiraia wa Sudan Jumatatu walitia saini makubaliano ya kisiasa ili kumaliza hali ya kukwama ya kisiasa na kuanzisha serikali ya mpito ya kiraia ya miaka miwili.

Abdel Fattah Al-Burhan, Kamanda wa Jeshi la Sudan, na Mohamed Hamdan Dagalo, Kamanda wa Jeshi la Usaidizi wa Haraka, wametia saini makubaliano hayo kwa niaba ya vikosi vya kijeshi.

Wakati huo huo, wawakilishi wa Muungano wa Makundi ya Uhuru na Mabadiliko, Muungano wa Mapinduzi, mashirika mengine ya kisiasa, vyama vya wafanyakazi na asasi za kiraia wametia saini makubaliano hayo kwa niaba ya makundi ya kisiasa.

Katika hotuba yake kwenye hafla ya kutia saini Al-Burhan ameapa kwamba jeshi litaachana na mchakato wa kisiasa na kuunga mkono mabadiliko ya kidemokrasia hadi kufikia uchaguzi mkuu.

Amesisitiza haja ya kuvifanyia mageuzi Vikosi vya Majeshi vya Sudan ili kuvifanya kuwa taasisi za kikatiba zinazozingatia katiba na kudumisha kutoegemea upande wowote bila ya kujihusisha siasa au upendeleo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka Mohamed Hamdan Dagalo amesisitiza dhamira yake ya kibinafsi na ya kitaasisi ya kulinda kipindi cha mpito na kuimarisha utawala wa kiraia.

"Makubaliano ya kisiasa, ambayo tumetia saini leo, unajumuisha awamu mpya katika historia ya kisiasa ya Sudan inayolenga kukamilisha kipindi cha mpito," Dagalo amesema wakati akihutubia hafla ya kutia saini.

Al-Wathiq Al-Birair, mwakilishi wa Muungano wa Makundi ya Uhuru na Mabadiliko, amesema makubaliano hayo "yanaanzisha utawala wa kiraia na kukamilisha majukumu ya Mapinduzi matukufu ya Desemba."

Makubaliano hayo ya kisiasa yanatokana na rasimu ya katiba ya mpito iliyotolewa na kamati ya uongozi ya Chama cha Wanasheria wa Sudan, ambayo ilikubaliwa duniani na nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi, huku vikosi hivyo vikielezea kutoridhishwa kwake na vifungu vyake kadhaa.

Rasimu hiyo inaweka mfumo wa kikatiba wa kusimamia kile kilichobaki katika kipindi cha mpito, na inatoa nafasi ya kuundwa kwa serikali inayoongozwa na raia na baraza la kuendesha masuala ya usalama na ulinzi wa taifa.

Sudan imekuwa ikikumbwa na msukosuko wa kisiasa tangu Al-Burhan atangaze hali ya hatari Oktoba 25, 2021 na kuvunja baraza kuu na serikali.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha