Kila Bandari Kenya Kuwa Na Mkurugenzi Wake Mkuu

() Mei 25, 2021

Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), inapanga kubadilisha usimamizi wa bandari ili kila moja iwe chini ya Mkurugenzi Mkuu wake.

Hii imefanya mchakato wa kuajiri Mkurugenzi Mkuu wa KPA kusimamishwa mara tatu ili mageuzi yatekelezwe.

Kuna bandari tatu muhimu Kenya ambazo ni Mombasa, Lamu na ile ya Kisumu ambayo imefanyiwa ukarabati.

Katika mpango huo, serikali inalenga kurekebisha usimamizi wa bandari za Kenya ambapo kila bandari inatarajiwa kuwa na Mkurugenzi wake mkuu. Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alisema kuwa shughuli hiyo ya kumteua mkurugenzi mpya wa KPA ilicheleweshwa kutokana na marekebisho na ukarabati unaoendelea katika bandari hizo.

Akizungumza na wanahabari, Bw Yatani alisema kuwa kando na ufunguzi rasmi wa bandari ya Lamu siku ya Alhamisi, serikali iko katika hatua ya mwisho ya kufanya maamuzi kuhusu jinsi kila bandari nchini itasimamiwa na Mkurugenzi wake kwa kuwa zote zinanatoa huduma maalum.

Vile vile, Bw Yatani alisema kuwa, ikiwa mpango huo mpya utapitishwa, kila bandari itaongozwa na mkurugenzi wake.

Kuingiliwa kwa mchakato huo na wanasiasa kumekuwa kukitajwa kuwa chanzo cha kusitisha uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa KPA.

Kulingana na duru, kuingiliwa na wanasiasa kumechangia kucheleweshwa kwa uteuzi wa mkurugenzi mpya wa KPA.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha