Kenya: Idadi Ya Vijana Kwenye Kilimo Na Ufugaji Ni Ya Chini Mno – Tafiti Za Shirika

(CRI Online) Mei 25, 2021

Idadi ya vijana wanaofanya shughuli za kilimo nchini ni ya chini mno, limesema shirika lisilo la kiserikali (NGO) kutoka Amerika na ambalo huwapiga jeki na kuwahamasisha.

Kwenye ripoti ya utafiti wa hivi karibuni ya Heifer International (HPI) uliojumuisha mataifa 11 barani Afrika, asilimia tisa pekee ya vijana wanafanya ufugaji wa kuku.

Ripoti hiyo pia inaeleza kwamba ni asilimia 12 ya idadi ya vijana ndio wanaendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Takwimu hizo zinatia wasiwasi, HPI ikionya endapo hatua mahususi hazitachukuliwa huenda sekta ya kilimo cha ufugaji siku za usoni ikafifia Kenya na Bara la Afrika kwa jumla.

Kwa mujibu wa Bw David Ojwang, meneja wa mikakati na programu katika Heifer Kenya, hali hii ilikuwa bayana katika nchi zote walizoshirikisha. Mbali na ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa, shughuli zingine za kilimo zilifuata mkondo huo – Idadi ya vijana wanaokiendeleza kuwa ya chini sana. Ojwang anasema kuwa hili ni jambo linalopaswa kutia wasiwasi, na watu kuungana kuliangazia,

Huku sekta ya kilimo ikiwa kati ya nguzo kuu za uchumi wa serikali, ikikadiriwa kubuni karibu asilimia 50 ya nguvukazi nchini, Ojwang anasema haja ipo kuwapa vijana motisha kuikumbatia kama njia ya kujiajiri.

Kwa mujibu wa utafiti wa HPI, vijana wengi wanaamini kilimo na ufugaji, kinapaswa kuendeshwa na waliostaafu na waliokula chumvi, wengine wakikumbatia kazi ambazo haziwachoshi kupata hela kama vile uendeshaji bodaboda.

(Wahariri wa tovuti:Shixi,Zhao Jian)

Picha