Bidco Yazidi Kupanua Biashara Zake Barani Afrika

(CRI Online) Juni 15, 2021

Kampuni ya Bidco Africa Ltd imeonyesha uwezo wake wa kujiendeleza barani Afrika hasa uwekezaji na ustawishaji wa viwanda.

Waziri Msaidizi wa Biashara (CAS) Bw David Osiany, alizuru kampuni hiyo ya Bidco Africa Ltd inayotengeneza sharubati na maji mjini Ruiru, na kupongeza wasimamizi kwa juhudi wanazofanya.

Alieleza kuwa ameridhika na jinsi kiwanda hicho kinavyotengeneza bidhaa zake ikiwemo kufuata maagizo yote ya Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa (KEBS).

Alitaja ushirikiano wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hasa wa Kenya na nchi jirani ya Tanzania kama njia mojawapo ya “kuinua uchumi wetu na wa nchi jirani”.

Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa katika kiwanda hicho cha Ruiru ni maji ya matunda – sharubati – chapa Jooz, na mengine aina tofauti, pamoja na maji safi ya kunywa.

Aliyasema hayo Jumatatu alipozuru kiwanda hicho na maafisa kadhaa kutoka wizara yake pamoja na maafisa wa ukaguzi wa bidhaa bora zinazotengenezwa viwandani.

Alieleza kuwa serikali inashauri viwanda vinavyowekeza nchini vifanye kweli kwa kutengeneza bidhaa zilizo na ubora wa hali ya juu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha