Kenya kutumia AfCFTA kuipiga jeki bandari ya Lamu

(CRI Online) Juni 18, 2021

Kenya inatarajia kutumia mkataba wa Biashara huru wa Bara la Afrika (AfCFTA) ili kupata biashara kwa ajili ya Bandari ya Lamu.

Nchi hiyo inalenga kutumia eneo Maalum la Kiuchumi (SEZ) karibu na bandari mpya kama kituo cha kuongeza thamani kwa bidhaa za kilimo miongoni mwao chai na kahawa, ambayo ni mauzo muhimu ya nje kwa Kenya.

Serikali pia inalenga usafirishaji wa parachichi na mifugo na viwanda vinavyotarajiwa kujengwa katika eneo hilo maalum la kiuchumi (SEZ) kwa ajili ya kuongeza thamani katika matunda ya makopo, mbogamboga na juisi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kukuza Usafirishaji na Chapa Kenya (KEPROBA), bandari ya Lamu na eneo maalum la kiuchumi (SEZ) pia zinatoa fursa kwa wawekezaji kufurahia idhini ya mizigo ya kuuzwa nje ya nchi kutolipiwa ushuru na kodi mbalimbali.

Vichocheo vingine ni pamoja na punguzo la asilimia 50 kwa gharama ya marubani, huduma za maboti na uelekezaji wa vyombo vya majini kwa kutumia Bandari ya Lamu, gharama ambazo kwa sasa zinatozwa kwa wastani wa Sh16,200, Sh32,400 na Sh21,600, mtawalia, katika Bandari ya Mombasa.

Mamlaka ya Mapato nchini Kenya (KRA) pia imepunguza ushuru wakati Mamlaka ya Bandari (KPA) imetoa hadi siku 30 kipindi cha kuhifadhia mizigo na magari.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha