Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lazindua mkakati wa Utalii

(CRI Online) Juni 18, 2021

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limeandaa mpango mkakati wa miaka mitano unaolenga kutekelezwa kwenye maeneo saba ikiwamo kubuni na kukuza wigo wa bidhaa na mazao ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini humo.

Kamishna Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete, alibainisha hayo jana kwenye semina iliyoandaliwa na shirika hilo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma.

Alisema shirika linatekeleza shughuli za uhifadhi na utalii kulingana na Mpango Mkakati wa miaka mitano (2018/19 – 2022/23) ambao umefanyiwa marejeo na kuandaa mkakati mwingine wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22-2025/26.

Shelutete alisema mkakati huo unalenga kutekeleza maagizo ya serikali katika sekta ya utalii nchini. Alitaja eneo lingine litakalopewa kipaumbele kwenye mkakati huo ni kuimarisha miundombinu ya utalii hususani barabara, viwanja vya ndege, malango, magati, malazi, mawasiliano, maji na umeme.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha