AfCFTA yaboresha mfumo wa malipo ili kuwezesha biashara barani Afrika

(CRI Online) Juni 21, 2021

Katibu Mkuu wa Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene amesema, uongozi wa Eneo hilo unaboresha mfumo wa malipo ili kuwezesha biashara kati ya nchi za Afrika.

Akizungumza na Shirika la Habari la China Xinhua, Bw. Mene amesema Mfumo wa Malipo na Mapatano wa Eneo hilo (PAPSS) utaanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu ili kuwezesha biashara kati ya nchi husika barani Afrika.

Ameongeza kuwa, mfumo huo ambao unaendelezwa mahususi kwa ajili ya malipo ya biashara kwa nchi za Afrika, unafanyiwa majaribio katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.

Wakati huohuo, Mene amesema baadhi ya changamoto katika makubaliano ya biashara zimechelewesha utekelezaji kamili wa Eneo hilo barani Afrika, lakini ameeleza matumaini yake nchi nyingine zitakamilisha makubaliano yao ili kuungana na nchi kama Kenya, Afrika Kusini na Misri ambazo tayari zimeanza kufanya biashara kupitia Eneo hilo.

(Wahariri wa tovuti:Li Yidan,Zhao Jian)

Picha