Real Madrid yashangazwa na Klabu ‘Kinda’ ya Sheriff huku Messi akifunga goli lake la kwanza tangu ahamie Paris

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 30, 2021

Miamba ya soka la Ulaya, Timu ya Real Madrid usiku wa kuamkia Jumatano imeangukia pua kwa Timu kinda ya Sherrif baada ya kufungwa magoli 2-1 kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Santiago Bernabeu jijini Madrid, Hispania katika michuano ya klabu bingwa za Ulaya kuwania kufuzu kuingia nafasi ya mtoano ya mzunguko wa pili.

Sherrif, klabu ya soka iliyoanzishwa mwaka 1997 kwenye mji usiyo na umaarufu wa Transnistria huko Moldovan na ikiwa haina rekodi kubwa kwenye michuano hiyo, iliwaduwaza Real Madrid ambao ni mabingwa mara 13 wa Ulaya kupitia magoli ya Djasur Yakhshibaev na Sebastien Thill yaliyofungwa dakika ya 25 na 90 sawia huku lile la kufutia machozi la Madrid likiwekwa wavuni kwa njia ya penati na Karim Benzema mnamo dakika ya 65 ya mchezo.

Naye Lionel Messi akiiongoza timu yake ya Paris Saint German kupata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Manchester City alikuwa mwenye furaha baada ya kufunga goli lake la kwanza tangu ajiunge na miamba hiyo ya soka la Paris akitokea Klabu ya Hispania ya FC Barcelona.

Matokeo mengine katika michezo hiyo ni pamoja na RB Leipzig 1-2 Club Brugge, AC Milan 1-2 Atletico Madrid, FC Porto 1-5 Liverpool, Ajax 1-0 Sporting CP, Borussia Dortmund 1-0 Sporting CP Shakhtar Donetsk 0-0 Inter Milan.

Aidha, usiku wa kuanzia leo Alhamisi michuano hiyo iliendelea tena ambapo matokeo yalikuwa kama ifuatavyo: Manchester United 2-1 Villarreal, Benfica 3-0 Barcelona, Juventus 1-0 Chelsea, Atalanta 1-0 Young Boys, Bayern Munich 5-0 Dynamo Kyiv, FC Salzburg 2-1 Lille, Wolfsburg 1-1 Sevilla na Zenit St. Petersburg 4-0 Malmoe FF. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha