Rais wa China atangaza kuanzisha Mfuko wa Viumbe Anuwai wa Kunming kusaidia nchi zinazoendelea

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 13, 2021

BEIJING - Rais Xi Jinping wa China Jumanne ya wiki hii ametangaza kuanzisha Mfuko wa Viumbe Anuai wa Kunming na mpango wa China wa kutoa yuan bilioni 1.5 (karibu dola za kimarekani milioni 233) kwenye mfuko huo.

Aidha, Rais Xi amesema kwamba, China inaharakisha ujenzi wa mfumo wa maeneo ya hifadhi sambamba na Mbuga za hifadhi za kitaifa za kudumu na kuongeza kwamba maeneo yenye umuhimu mkubwa wa mfumo wa kiasili wa ikolojia na yenye mazingira ya kipekee, maeneo yenye urithi wa kiasili na maeneo yenye hifadhi ya viumbe anuai yatahusishwa kwenye mfumo huo.

Rais Xi alitangaza mpango huo wakati alipohutubia kwa njia ya video Mkutano wa kilele wa mkutano wa 15 nchi zilizotia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Viumbe Anuai unaofanyika Kunming Mji Mkuu wa Mkoa wa Yunnan, Kaskazini Magharibi mwa China. Amesema, Mfuko huo utatumika kusaidia ulinzi wa viumbe anuai katika nchi zinazoendelea.

“China inatoa wito na inakaribisha pande zote kutoa mchango kwenye mfuko huo” Xi amesema.

Juu ya uanzishaji wa mfumo wa maeneo ya hifadhi, China imepiga hatua kubwa katika kujenga ustaarabu wa kiikolojia, pamoja na uhifadhi wa wanyamapori, alisema Xi, akitoa mfano wa safari ya hivi karibuni ya tembo wanaotangatanga katika mkoa wa Yunnan Kusini Magharibi mwa China.

Rais Xi amesema, pamoja na maeneo ya ardhi ya hifadhi ya kilometa za mraba 230,000, kundi la kwanza la mbuga za taifa za China lina karibu asilimia 30 ya spishi muhimu za wanyamapori na mimea nchini humo.

Maendeleo ya ustaarabu wa kiikolojia yanapaswa kuchukuliwa kama mwongozo wa kuratibu uhusiano kati ya binadamu na viumbe asili, Rais Xi alisema, akiongeza kuwa shughuli za binadamu zinapaswa kuwekwa ndani ya mipaka ya ikolojia na mazingira.

Kwa upande wa viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo kwa njia ya video, wametaka uhamasishaji wa kimataifa, makubaliano mapana na hatua madhubuti za kuhifadhi viumbe anuwai.

"Jaribio letu la karne mbili la kuchoma mabaki ya mafuta, kuharibu misitu, nyika na bahari, na kuharibu ardhi, limesababisha janga la baiolojia," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema katika hotuba yake.

Mkuu huyo wa UN alielezea kuingiliwa kwa viumbe asili na shughuli za binadamu ni "vita vya kujiua" na akasisitiza kwamba "tunapoteza”.

Katika hotuba yake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitoa wito wa kupitishwa kwa mfumo kabambe wa kimataifa unaokidhi changamoto na matarajio ya jamii anuwai.

"Ni juu ya kizazi chetu kubadili mwenendo na kurudisha harambee nzuri na viumbe asili" alisema.

Rais wa Russia Vladimir Putin amebainisha kuwa "malengo ya uhifadhi wa uoto wa asili hayawezi kushughulikiwa vyema na nchi yoyote peke yake. Hii ni kazi ya kawaida kwa nchi zote, kwa binadamu wote, bila kutia chumvi."

Mkutano wa 15 wa nchi zilizosaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu Viumbe Anuai unaojulikana kama COP15, kwa mwaka huu wa 2021 unabeba kaulimbiu ya "Ustaarabu wa Kiikolojia: Kujenga Hatma ya Pamoja ya Viumbe hai Duniani". COP15 ni mkutano wa kwanza wa dunia ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa ukionesha ustaarabu wa kiikolojia, ambayo ni falsafa iliyopendekezwa na China. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha