Uamuzi wa mahakama ya UN juu ya mgogoro wa mpaka waleta maoni kinzani kutoka Kenya, Somalia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 14, 2021

Uamuzi wa Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa juu ya mgogoro wa mpaka wa baharini kati ya Kenya na Somalia umepokelewa kwa maoni tofauti baina ya nchi hizo mbili jirani za Afrika Mashariki.

Jumanne ya wiki hii Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ) imeamua kwamba hakukuwa na mpaka wowote wa bahari uliokubaliwa na kuipendelea zaidi Somalia ambayo itapata sehemu kubwa ya eneo la kilomita za mraba 100,000 katika Bahari ya Hindi, eneo ambalo lina uwezekano wa kuwa na utajiri wa gesi na mafuta.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema nchi yake iko tayari kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro huo, amekataa uamuzi huo, akisema Nairobi ina wasiwasi na utekelezaji wa uamuzi huo na athari zake kwa eneo la Pembe ya Afrika na Sheria ya Kimataifa kwa jumla. "Kenya inapenda kuonesha kwamba inakataa kabisa na haitambui matokeo katika uamuzi huo."

Kenyatta huku akisistiza ICJ haikuwa na mamlaka kusikiliza kesi hiyo, alishutumu ICJ kwa ukosefu wa haki na upendeleo kwa kukataa kuruhusu Kenya kutumia njia zote za kikanda za utatuzi wa mgogoro, licha ya kuwepo kwa mfumo thabiti wa kisheria wa Umoja wa Afrika (AU) juu ya utatuzi wa masuala ya mipaka na mgogoro.

Hata hivyo, Rais wa Somalia Farmajo katika hotuba ya televisheni kwa taifa Jumanne jioni, amesema uamuzi huo ni ushindi wa kihistoria kwa Wasomali wote na unaonesha uadilifu na uwazi wa ICJ. "Serikali ya Somalia hapa inathibitisha kwamba tunakubali uamuzi wa Mahakama, kulingana na sheria na kanuni za kimataifa. Tunatumai kuwa serikali ya Kenya itaheshimu sheria za kimataifa na itaacha kuendeleza upotoshaji na kutokufuata sheria” amesema.

Wachambuzi wa mambo wa eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wanasema uamuzi wa Mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa unaweza kuharibu uhusiano dhaifu kati ya nchi hizo jirani kwa kuwa Kenya ni mchangiaji mkubwa wa wanajeshi wanaosaidia serikali ya Somalia katika vita dhidi ya kundi la al-Shabab. Inaweza pia kuwa na athari kubwa za usalama na uchumi katika siku za usoni. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha