China yarusha setilaiti yake ya kwanza ya uchunguzi wa jua

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 15, 2021
China yarusha setilaiti yake ya kwanza ya uchunguzi wa jua

Baada ya kuweka vyombo vya uchunguzi wa mwezi na Sayari ya Mars, China imeanza kuweka vyombo vyake vya uchunguzi kwenye jua.

Katika hatua ya kihistoria, nchi hiyo imerusha setilaiti yake ya kwanza ya uchunguzi wa jua Alhamisi ya wiki hii, ikilenga kuwasaidia wanasayansi kukuza ujuzi wao kuhusu jua.

Setilaiti ya China ya uchunguzi wa jua yenye uzito wa kilo 508 imerushwa na roketi ya Long March-2D saa 6:51 jioni kutoka Kituo cha urushaji wa Setilaiti cha Taiyuan, mkoani Shanxi na kisha ikaingia kwenye mfumo wa mzunguko wa jua kilomita 517 mbali na Dunia, idara ya Anga ya juu ya China imesema.

Mamlaka hiyo imesema, setilaiti hiyo inatarajiwa kuwapa wanasayansi takwimu za kwanza za kiwango cha juu kuhusu uchunguzi wa eneo la chanzo cha mlipuko wa jua na itaboresha uwezo wa utafiti wa China katika fizikia ya jua, na kuongeza kuwa urushaji wa setilaiti hiyo una maana sana kwa uchunguzi wa anga ya juu ya China na teknolojia ya setilaiti.

Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Uhandisi ya Setilaiti ya Shanghai katika Chuo cha Teknolojia ya Anga ya juu cha Shanghai Bw.Wang Wei amesema chombo hicho ni darubini ya kwanza ya jua ya China na imebuniwa kufanya kazi kwa angalau miaka mitatu.

 "Kisayansi, chombo hicho kinaweza kuchunguza na kurekodi mabadiliko ya mambo ya fizikia kwenye jua kama vile joto na kasi yake, na kuwarahisisha wanasayansi kuchunguza mienendo na fizikia wakati wa mlipuko wa jua." Wang amesema.

Zhao Jian, afisa mwandamizi katika idara ya anga ya juu ya China anayesimamia mpango wa setilaiti, alisema ni muhimu kwa binadamu kufahamu jua kwa sababu shughuli za jua zina athari nyingi kwa maisha ya binadamu kwenye dunia. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha